Kinana: Lowassa safi, Nyalandu anazurura

Saturday March 14 2015

“Mfano ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye

“Mfano ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye anafanya kazi ya kuzunguka nchi nzima na maeneo mengine wakati mizunguko yake haisaidii kuondoa matatizo ya wananchi.” Kinana 

By Habel Chidawali, Mwananchi

Kondoa/Monduli. Jana ilikuwa siku ya hisia tofauti kwa watu wawili wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais, Edward Lowassa na Lazaro Nyalandu baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kumsifu mmojawao na kumponda mwingine.

Akiwa Kondoa, Kinana alitumia muda mwingi kujibu kilio cha wananchi wanaosumbuliwa na askari wa wanyamapori kwa kumponda Waziri Nyalandu kuwa anazurura bila kushughulikia matatizo ya wananchi, lakini saa chache baada ya kuwasili Monduli alimsifu Lowassa kuwa ni kiongozi shupavu.

Tayari Nyalandu ameshatangaza nia ya kugombea urais, wakati Lowassa, mmoja wa wanachama wa CCM wanaotajwa sana kwenye kinyang’anyiro hicho, hajatangaza uamuzi wake lakini anatumikia adhabu ya chama chake kilichomfungia kujihusisha na harakati za uongozi pamoja na makada wengine watano.

Baada ya msafara wa Kinana kuwasili Monduli na kupokewa na viongozi wa chama hicho wa eneo, katibu huyo wa CCM, Kinana alipata nafasi ya kuzungumza machache kabla ya kuanza safari ya kukagua shughuli mbalimbali.

“Hatuna shaka na Monduli kwa kuwa yupo kiongozi shupavu, ndugu yetu Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa (Halmashauri Kuu ya CCM) Nec,” alisema Kinana akiwaelezea wananchi waliokuwapo eneo hilo.

“Wa Monduli mna kiongozi shupavu na mchapakazi. Hongera Bwana Lowassa.”

Baadaye, Lowassa aliwakaribisha akisema: “Mmefanya kazi kubwa sana ya kukijenga chama chetu. Nawashukuru sana, karibuni.”

Naye katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Nafurahi kuwa katika jimbo la mzee wangu, rafiki yangu Edward Lowassa. Mapokezi mazuri, bila shaka Arusha mmeamka.”

Kinana amekuwa akitumia sehemu kubwa ya ziara yake kushuhutumu viongozi wa Serikali na hasa mawaziri kwa kushindwa kuwatatulia wananchi matatizo yao na ilifikia wakati aliwataja mawaziri wanne aliowaita kuwa ni mizigo, tofauti na alivyofanya kwa waziri mkuu huyo wa zamani.

Lowassa alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne na anajulikana kama mtu aliye tayari kufanya uamuzi mgumu. Alilazimika kujiuzulu wadhifa huo mwaka 2008 baada ya kuibuka kwa kashfa ya Richmond.

Kinana alikuwa mtu tofauti wakati akijibu kero za wananchi mkoani Singida, ambako alimtaja moja kwa moja Waziri Nyalandu kuwa hashughulikii matatizo ya wananchi na badala yake amekuwa akizunguka bila msaada wowote.

Kinana alisema hayo juzi katika Kijiji cha Ikengwa, Kata ya Kinyasi wilayani Kondoa baada ya wananchi wa kijiji hicho kumchongea Nyalandu kwa Kinana kwamba wizara yake inawaua na kuwaumiza bila ya hatia, hivyo wamechoka.

Wananchi hao walisema mateso wanayoyapata kutoka kwa askari wa wanyamapori katika Pori la Mkungunero ni makubwa ambayo yanalenga kuondoa uhai wa watu.

Katibu wa CCM wa Kata ya Inyasi, Jusberi Jumanne aliyesoma risala ya malalamiko hayo, alisema wanaishi ndani ya kijiji chao na kufanya shughuli zao za kilimo, lakini kila wakati wanachomewa nyumba, mazao yao kufyekwa na hata kuwasababishia ulemavu na vifo.

“Mheshimiwa katibu mkuu, hapa ni kijiji halali kilichosajiliwa 1974 na kupewa hati 398, lakini hifadhi hiyo ilikuja kuweka mipaka yao mwaka 2006, jambo hili sisi tunaona ni uonevu ambao tunafanyiwa  bila ya kushirikishwa na kuambiwa tuhame kwa nguvu na hatujui mahali pa kwenda,” alisema.

Akijibu hoja hiyo Kinana alionekana kukerwa  na namna maisha ya watu wa maeneo hayo yasivyoshughulikiwa ili nao waishi kama Watanzania wengine.

“Ni jambo la aibu kwa Waziri wa Maliasili na Utalii kusikia migogoro lakini yeye akawa kimya,”alisema Kinana.

“Nyalandu awaeleza Watanzania kama kuna mahali amefanikiwa kumaliza kabisa migogoro walau 10 kwani amekuwa ni bingwa wa maneno na matembezi.”

Kinana alisema ni lazima Nyalandu  abebe msalaba huo kwani roho za binadamu zina thamani… ni heri roho ya binadamu kuliko mnyama ingawa alizuia wanyama wasiuawe.

“Hawa mawaziri lazima waje, na nina wasihi waje haraka, yaani Waziri wa Maliasili na Utalii na mwenzake wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,” alisema.

“Mfano ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye anafanya kazi ya kuzunguka nchi nzima na maeneo mengine wakati mizunguko yake haisaidii kuondoa matatizo ya wananchi.”

Kinana alitaka kamatakamata ya wananchi isimamishwe kwanza hadi ufumbuzi kuhusu mipaka ya pori hilo itakapoangaliwa upya. Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Waziri Nyalandu alisema anakubaliana na alichosema Kinana, lakini akataka watu wajjue kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu.

“Mgogoro huo ni wa siku nyingi, hivyo busara inahitajika sana kulinda watu, mali zao na maliasili. Niliunda kamati ambayo yumo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na Manyara, Ma-RAS (maofisa utawala wa mikoa) wao na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambayo imefanya uchunguzi pamoja na kuongea na wananchi,” alisema.

“Kamati inatarajiwa kumaliza kazi wiki hii na itanikabidhi kwa kuwa mimi ndiye niliyeiunda. Nimepanga kwamba ndani ya hizi wiki mbili za Bunge, mimi na Waziri wa Ardhi tutatangaza suluhisho la tatizo hili. Tutaenda pamoja  Mkungunero kuongea na wananchi.”

Katika mkutano huo, Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita alisema kuwa katika kata hiyo na maeneo mengine kumekuwa na kelele zinazotishia amani na tayari kwa baadhi ya watu wameshapoteza maisha.

Walimkabidhi Kinana maganda ya risasi pamoja na rundo la mabaki ya nguo zilizochomwa moto na askari wa wanyamapori.

Advertisement