Kinyozi atoa ofa ya kuwanyoa bure Trump, Kim Jong Um

Mwananchi wa Vietnam, Nguyen Huu Thien akinyolewa nywele kwa staili ya Kim Jong Un katika saluni moja mjini Hanoi leo. AFP

Muktasari:

Tangu atangaze ofa hiyo, kinyozi huyo ameshapata wateja 200 waliotaka kunyoa staili ya Kim wakati watano tu ndio waliotaka staili ya Trump

 

Kinyozi mbunifu wa Hanoi amesema yuko tayari kuwanyoa bure viongozi wa mataifa makubwa mawili duniani, Kim Jong Un wa Korea Kaskazini na Donald Trup wa Marekani kabla ya marais wao kukutana Vietnam wiki ijayo.

Kim hunyoa nywele zake pembeni na kuacha za utosini, wakati Trump huachia nywele zake za rangi ya kimanjano na shaba.

Kinyozi huyo, Le Tuan Duong amekuwa akizidiwa na wateja tangu tangu atangaze offa hiyo, ambayo ni ishara ya kuonyesha kufurahishwa kwake na viongozi hao mahasimu watakaokutana Februari 27-28 mjini Hanoi.

Lakini staili moja ya nywele imekuwa maarufu.

"Katika kipindi cha siku tatu, nimenyoa kwa staili ya nywele ya Kim watu 200, lakini ni watu watano tu waliopenda staili ya Trump," aliiambia AFP katika shule yake ya masuala urembo ya Tuan Duong mjini Hanoi.

Kinyozi huyo hutoza dola 43 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh80,000 za Kitanzania) kwa mtu anayetaka staili ya Trump ambayo huhusisha kupaka rangi, lakini kiwango hicho ni kikubwa kwa wananchi wa jiji hilo kunyoa hugharimu fedha kidogo.

Pamoja na staili ya Trump kutopendwa, baadhi ya wakazi wa Hanoi anafurahishwa nayo.

"Nataka wananchi wa Vietnam kumjua zaidi Trump, kwa kupitia staili yangu ya nywele. Kwangu Trump ni mtu mzuri na ndio maana nataka staili yake ya nywele," alisema Vuong Bao Nam, ambaye ndio kwanza alikuwa ametoka kutia rangi nywele.

Kinyozi huyo si msanii pekee jijini Hanoi ambaye anapenda viongozi.

Mchoraji anayeitwa Tran Lam Binh amekuwa akihangaika kuchanganya rangi kuchora picha za vichwa vya viongozi hao wawili kutuma ujumbe wa amani, ikiwemo moja iliyozungukwa na mchoro wa moyo wa rangi nyekundu iliyoandikwa "L-O-V-E (pendo)".

"Nataka sana viongozi hawa wawili, au angalau mmoja, aje na kuona kazi zangu hapa... Naota kuwapa moja ya picha hizi," Binh aliiambia AFP akiwa mgahawani jijini Hanoi ambako amekuwa akifanyia kazi picha hizo.

Msanii huyo ambaye anajiita Trump, alianza kuchora picha za kiongozi huyo wa Marekani baada ya uchaguzi na tayari ana picha 50 za sura yake, baadhi ya hizo alizionyesha nje ya Ikulu ya Marekani jijini Washington.

"Wakati napomchora hujisikia kama nazielewa hisia zake za ndani kwa kupitia macho yake, sura yake," alisema mchoraji huyo mwenye umri wa miaka 36 akiwa amesimama pembeni ya michoro yake kadhaa.

Mkutano huo baina ya Trump na Kim unalenga katika kuendeleza waliyoongea katika mkutano wao uliofanyika Juni nchini Singapore, ukiwa ni mkutano wa kwanza wa aina yake baina ya viongozi wa Marekani na Korea kaskazaini tangu vita vya Korea vya mwaka 1950-53.