Kiongozi wa mwenge agoma kuzindua kituo cha afya

Muktasari:

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Mzee Mkongea Ali ameshindwa kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha kata ya Munzeze wilayani Buhigwe, kutokana na eneo hilo la mradi kuwepo kwa makazi ya wananchi.

Buhigwe. Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Mzee Mkongea Ali ameshindwa kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha kata ya Munzeze wilayani Buhigwe mkoani Kigoma baada ya kuwepo makazi ya watu katika eneo la kituo hicho.

Akizungumza leo Ijumaa Aprili 19, 2019 katika kijiji cha Munzeze wakati alipotembelea kituo hicho kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi, Ali amesema eneo hilo ni la Serikali wananchi hawakutakiwa kuishi hapo.

Kiongozi huyo amemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo (DED), Anosta Nyamoga kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo na eneo hilo libaki kuwa la Serikali na si wananchi kuweka makazi yao.

Awali, akipokea mwenge, mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayalina amesema mwenge huo upo katika wilaya yao na kwamba wananchi wajitokeze kwa wingi kwani ni ishara ya kuwaunganisha pamoja kama Watanzania.

"Katika wilaya yetu mwenge utakimbizwa katika kata nane ambazo zina miradi ya maendeleo ambayo kuna baadhi itawekwa jiwe la msingi na mingine kuzinduliwa,” amesema Ngayalina.

Mbio za mwenge kimkoa zimekimbizwa wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi minane, mbalimbali ya maendeleo katika kata nane kati ya 20. Miradi hiyo ina thamani ya zaidi ya Sh800 milioni.