Kipigo Chelsea chamuibua kocha Arsenal

Baada ya kuifunga Chelsea mabao 2-0, kocha wa Arsenal, Unai Emery amesema kikubwa kwenye kikosi chake ni kuhakikisha anakuwa na uwiano mzuri wa namna ya kucheza michezo ya nyumbani na ugenini.

Emery alisema amefurahishwa na matokeo waliyopata pamoja na pointi tatu muhimu, baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya West Ham United katika mchezo uliopita.

“Nadhani tumeimarika. Tunaweza kuwa na timu nzuri zaidi katika siku chache zijazo, lakini kwa sasa tunatakiwa kuwa na uwiano wa uchezaji katika michezo yetu ya nyumbani na ugenini.

“Nimefurahishwa na dakika 20 za mwisho tulivyokuwa tukijilinda. Kipindi cha kwanza kilitofautishwa na matokeo, lakini kipindi cha pili tulionyesha namna tunavyoweza kuzuia pamoja,” alisema kocha huyo.

Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri ambaye amechukizwa na kipigo hicho cha pili ndani ya michezo mitatu ya hivi karibuni, alisema amevunjika moyo na namna ambavyo wachezaji wake walivyopoteza hamasa ya kupambana.

Sarri alisema kilichotokea kwa wachezaji wake ni kama kile ambacho kilitoa fursa kwao kupoteza bao 1-0 katika mchezo wa kombe la Ligi dhidi ya Tottenham Hotspurs kwenye Uwanja wa Wembley, London.

“Mtazamo wa kupigania matokeo ndicho kilichotuangusha kuliko kitu kingine chochote kile. Tunatakiwa kuondokana na hilo, niseme wazi kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa katika hamasa ya kucheza kwa nguvu kwa kila mchezo.

“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri. Hatukucheza kabisa soka letu kwa sababu tulikosa umoja wa uchezaji, hasa katika eneo la penalti, ukiangalia bao la kwanza ni mfano dhahiri,” alisema kocha huyo Mtaliano.

Mabao ya Arsenal katika mchezo huo, yalifungwa na Alexandre Lacazette dakika ya 14 na beki wa kati, Laurent Koscielny dakika ya 39.

Ushindi wa Arsenal ni wa pili mfululizo katika mashindano yote dhidi ya Chelsea kwenye uwanja wa Emirates. Nayo Manchester United iliendeleza wimbi la ushindi, baada ya kuigagadua Brighton mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Liverpool ikiwa Anfield iliichapa Crystal Palace mabao 4-3 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 60.