Kisena wa UDA, Wambura wa TFF kortini

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakiumu Mkazi wa Kisutu jana ilikuwa na shughuli nyingine ya kupokea vigogo wa maeneo mbalimbali baada ya kigogo wa Udart na TFF kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Vigogo hao ni Simon Kisena, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni inayotoa huduma ya mabasi ya mwendo kasi ya Udart, na Michael Wambura, ambaye alikuwa makamu wa rais wa TFF kabla ya kufungiwa maisha kujiuhusisha na mchezo huo.

Kutokana na makosa yao kuwa hayana dhamana, washtakiwa katika kesi hizo watakuwa mahabusu hadi hapo hukumu itakapotolewa.

Katika kesi hiyo, waendesha mashtaka waliowasomea mashtaka Kisena na wenzake ni wanasheria wa Serikali, George Barasa, Esther Martin na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Imani Mizizi.

Wakati Kisena na wenzake watatu wakisomewa mashtaka 19, Wambura alisomewa mashtaka 17 na wote hawakupewa dhamana na hivyo kuanza maisha ya mahabusu jana.

Kesi ya Kisena

Mbali na Kisena, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Simon Kisena ambaye ni mhasibu wa Udart, Charles Selemani Newe na raia wa China, Chen Shi.

Wanashtakiwa kwa tuhuma za kuongoza mtandao wa uhalifu, mashtaka manne ya kughushi nyaraka, mashtaka manne ya kuwasilisha nyaraka za uwongo na mashtaka manne ya utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh2.4 bilioni.

Mashtaka mengine ni kujenga kituo cha mafuta bila kibali cha Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) na kuuza mafuta mahali pasiporuhusiwa (makao makuu ya kampuni hiyo- Jangwani).

Pia wanakabiliwa na mashtaka ya kujipatia zaidi ya Sh1.1 bilioni kwa njia za udanganyifu; kuisababishia Udart hasara ya zaidi Sh2.4 bilioni, na wizi wa mafuta yenye thamani ya zaidi ya Sh1.2 bilioni mali ya Udart.

Pia wanadaiwa kughushi nyaraka kwa lengo la kuonyesha kwamba washtakiwa hao ni wanahisa katika kampuni ya Longway Engineering na kwamba waliridhia kufunguliwa kwa akaunti hiyo KCB kuwasilisha nyaraka hiyo katika benki hiyo.

Vilevile wanadaiwa kughushi nyaraka kwa udanganyifu kuhamisha zaidi ya Sh1.3 bilioni kutoka akaunti iliyofunguliwa KBC, kama malipo kwa kampuni ya Longway Engineering kwa ajili ya shughuli mbalimbali, kama ujenzi wa uzio wa vituo vya Kimara na Kivukoni.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari Mosi 2011 na Mei 2018, katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko eneo la Jangwani, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kisena na wenzake hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa katika hatua hizo za awali zakukamilisha taratibu za msingi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Kutokana na upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi haujakamilika, wakili wa washtakiwa hao, Majura Magafu ameiomba mahakama ielekeze kuharakishwa kwa upelelezi ili kesi hiyo iendelea katika hatua nyingine.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 25 itakapotajwa tena.

Ilivyokuwa kwa Wambura

Hali ilikuwa kama hiyo kwa Wambura, ambaye kwa nyakati tofauti ameiongoza TFF (enzi hizo FAT), akiwa katibu mkuu, Simba na pia mkoa wa Mara, alikokuwa mwenyekiti wa soka.

Baada ya kusomewa mashtaka ya utakatishaji fedha katika kesi uhujumu uchumi namba 10/2019, Wambura hakutakiwa kujibu chochote kutokana na kosa lake kuwa juu ya uwezo wa mahakama hiyo.

Wambura alisomewa mashtaka yake na jopo la wanasheria watatu wa Takukuru, George Barasa, Moza Kasubi na Imani Nitumezizi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kelvin Mhina.

Katika mashtaka hayo 17 dhidi yake, moja ni la kughushi, moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Barasa alidai mshtakiwa anadaiwa kughushi Julai 6, 2004 akiwa jijini Dar es Salaam. Amedai siku hiyo, Wambura aliandaa barua ya kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni mtendaji mkuu wa kampuni ya Jeck System na hivyo kudai arejeshewa dola 30,000 za Kimarekani ambazo kampuni hiyo iliikopesha taasisi hiyo ya soka pamoja na riba.

Pia mshtakiwa anatuhumiwa kutoa barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga, akionyesha kuwa dola 30,000 pamoja na riba ambazo pia aliikopesha taasisi hiyo, akijua kuwa si kweli.

Kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia zaidi ya Sh95 milioni kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya fedha mbalimbali na riba kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa si kweli.

Pia anadaiwa kujipatia Sh10 milioni kwa njia ya udanganyifu Juni 17, 2015 akiwa ofisi za TFF, akionyesha kuwa ni sehemu ya malipo ya dola 30,000 pamoja na riba kwa Jeck System, jambo ambalo si kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, wakili Kasubi alidai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, akiwa makao makuu ya shirikisho hilo, alijipatia Sh 25milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia anadaiwa kuwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh75.9 milioni kutoka TFF wakati akijua fedha hizo si halali na zimetokana na kughushi.

Barasa alidai kuwa upelelezi katika kesi bado haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Lakini wakili wake, Majura Magafu aliomba kesi hiyo itupiliwe mbali kwa kuwa mashtaka yote yalitakiwa yafunguliwe kama mashtaka ya kesi ya kawaida ya jinai na si uhujumu uchumi.