Kisena wa Udart, wenzake wafutiwa mashtaka

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia mashtaka Mkuugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena na wenzake watatu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu leo Jumatano Mei 15, 2019 imewafutia mashtaka Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena na wenzake watatu .

Kisena na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 19 likiwemo la utakatishaji wa fedha na kuusababishia mradi wa Udart hasara ya zaidi ya Sh2.41 bilioni.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Kisena, Charles Newe na raia wa China, Cheni Shi.

Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai(CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili wa Serikali, Grory Mwenda amedai mahakama hapo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea nalo dhidi ya washtakiwa hao .

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema shauri hilo lilikuja chini ya kifungu namba(91) cha CPA sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Amesema kutokana na maombi hayo mahakama hiyo imewafutia kesi.