Kishindo cha Saa nne za Makamba, Biteko Nyamongo

Sunday May 19 2019

 

By Peter Saramba, Mwananchi [email protected]

Tarime. Kilio cha tangu mwaka 2008 cha wakazi wa Nyamongo wilayani Tarime kuhusu maji yenye kemikali kutiririka kwenye makazi yao kutoka bwawa la maji machafu mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara sasa kimefika Serikalini.

Hii ni baada ya Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutangaza kuilima faini ya Sh5.6 bilioni mgodi huo kwa kutiririsha maji yenye kemikali kwenye makazi, vijito na mito.

Kwa lugha ya kawaida, hii inaweza kuwa ni kishindo cha ziara ya saa nne na nusu mgodini hapo ya Mawaziri, January Makamba Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Dotto Boteko wa Madini.

Ziara ya viongozi hao mgodini hapo ilianza saa 6:00 mchana na kukamilika saa 10:30 alasiri ya Mei 16, 2019.

Akitangaza uamuzi wa mgodi huo kulimwa faini juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Dk Samuel Gwamaka alisema kasoro zilizobainika pia zinatakiwa kurekebishwa ndani ya muda wa wiki tatu.

Mgodi huo pia umeagizwa na kujenga bwawa mbadala kudhibiti maji taka yenye kemikali yasiingie kwenye makazi ya watu na kuathiri maisha ya binadamu na mazingira.

Advertisement

Kabla ya uamuzi huo kutangazwa, Mawaziri hao wakiambatana na Wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais, Tume ya Madini, Wizara za Maji, Madini, Ardhi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na uongozi wa mgodi walishuhudia maji yanavyovuja na kuingia kwenye makazi ya watu.

Askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Charles Range ni miongoni mwa wananchi waliojitokeza mbele ya viongozi hao na kueleza wanavyoathiriwa na maji yenye kemikali yanayoingia kwenye makazi na vyanzo vya maji.

“Kuna vifo vya watu na mifugo vinavyodaiwa kusababishwa na madhara ya maji yenye kemikali, mazao na mazingira pia yameathirika. Wananchi tumeanza kupoteza imana kwa Serikali kutokana na tatizo hilo kudumu tangu mwaka 2008 bila ufumbuzi,” alisema Range

Akizungumza mbele ya Mawaziri na Wataalam wa Mazingira, Meneja wa Usalama, Afya na Mazingira wa mgodi huo, Reuben Ngusaru alikiri maji hayo kugundulika kutiririka kwenye makazi na kwamba juhudi za kuyadhibiti maji zinafanyika akitaja uchimbaji wa mitaro kuzunguka bwawa la maji taka kuwa miongoni mwa juhudi hizo.

“Pia tunatumia utaalam wa kupunguza maji kwenye bwawa kwa njia ya mvuke; njia hii inapunguza ujazo na mkandamizo wa maji bwawani ili yasipenye ardhini," alisema Ngusaru

Kupitia njia hiyo, Ngusaru alisema zaidi ya galoni 4, 000 za maji zinapunguzwa kila siku na hivyo kufanya bwawa lisielemewe.

Baada ya kushuhudia tatizo hilo, kusikiliza kilio cha wananchi na majibu ya uongozi wa mgodi, viongozi hao walijifungia kwenye kwa saa mbili na nusu kwenye kikao kilichoshirikisha viongozi wa Serikali, Wataalam na uongozi wa mgodi.

Hata hivyo uongozi wa mgodi ulitolewa ukumbini kupisha majadiliano kati ya Mawaziri na wataalam kabla ya kuitwa tena mwishoni mwa kikao.

Wakizungumza na Waandishi wa habari kwa kupokezana eneo la Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Tarime juzi, Makamba na Biteko walisema Serikali haifurahii kuwaadhibu, kuwapiga faini au kufungia shughuli za wawekezaji, lakini inapobidi hulazimika kuchukua hatua kulinda sheria, usalama, maisha ya wananchi na mazingira.

"Tunapenda mrabaha. Tunapenda mapato yatokanayo na dhahabu; lakini tunapenda zaidi usalama na maisha ya wananchi na mazingira yetu," alisema Makamba

Alionya kuwa Serikali itasitisha kwa muda au kufuta kabisa leseni ya kuendesha mabwaya ya maji taka ya mgodi huo iwapo kasoro zilizobainika hazitarekebishwa kwa muda uliotolewa.

"Mgodi hautafungwa kwa sababu hakuna tatizo kwenye shughuli za uchimbaji. Tutasitisha leseni ya kuendesha mabwawa na ikibidi tutaufuta kabisa," alisema Makamba.

Kwa upande wake, Biteko aliwataka wawekezaji wote katika sekta ya madini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za afya, mazingira na tozo mbalimbali za Serikali huku akisisitiza kuwa atakayekiuka ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Tatizo la uharibifu wa mazingira unaodaiwa kufanywa na mgodi huo umewahi kushughulikiwa na Kamati kadhaa ikiwemo ile ya Bunge ya Mazingira zilizokuwa zikiongozwa na waliokuwa Wenyekiti, Job Ndugai ambaye sasa ni Spika wa Bunge la Jamhruri ya Muungano na James Lembeli.

Advertisement