Kishindo cha siku mbili za Magufuli Mwanza

Mwanza. Siku mbili za ziara ya Rais John Magufuli mkoani Mwanza siyo tu zimeacha kishindo kwa viongozi, watendaji na watumishi wa umma katika maeneo aliyotembelea, bali pia imetoa matumaini kwa wananchi kutokana na maagizo na maelekezo aliyotoa.

Rais Magufuli aliyeingia mkoani Mwanza juzi mchana kupitia Sengerema alitoa maagizo mbalimbali yakiwamo kuharakisha mchakato wa msamaha wa kodi kwa makontena 56 ya bidhaa za ujenzi wa chelezo jana hiyohiyo na makontena hayo yawe yamefika Mwanza ndani ya wiki moja kuanzia jana.

Pia, aliagiza kukamilika haraka kwa ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli mbili za Mv Victoria na Mv Butiama.

Rais Magufuli alitoa maagizo kuhusu makontena hayo alipozunguza kwa simu kwa Katibu Mkuu wa Hazina, Dotto James baada ya taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Meli Tanzania (MSCL), Erick Hamisi kuwa makontena hayo yamekwama Katika Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi mmoja kutokana na mchakato wa msamaha wa kodi kutokamilika.

“Umeshazungumza na katibu mkuu wa uchukuzi? Wasiliana na katibu mkuu mwenzako wa uchukuzi, pamoja na kamishna mkuu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) muyamalize leo (msamaha wa kodi upatikane) na vifaa hivyo vianze kuja,” alisema Rais Magufuli akimwagiza James kwa simu.

“Leo ni tarehe ngapi? Leo tarehe 16 (Julai 16, 2019 - jana) nataka kabla ya tarehe 20 (Julai 20, 2019) vifaa hivyo viwe vimefika hapa (Mwanza), umenielewa katibu mkuu?”

Hata mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alionja joto la jiwe mbele ya Rais Magufuli baada ya kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha ya kwa nini jengo la wodi ya wanaume katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ya Butimba ilioanza kujengwa mwaka mmoja iliyopita haijakamilika.

Mongella alitakiwa kutoa maelezo baada ya Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba kushindwa kufanya hivyo.

Baada ya kutoridhishwa na maelezo ya Mongella na Kibamba, Rais Magufuli aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha jengo hilo linakamilika kabla au ifikapo Julai 30, 2019.

Maagizo mengine

Walionza kuonja joto ya jiwe wakati wa ziara ya Rais Magufuli mkoani Mwanza ni mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED), Magesa Mafuru ambao walibanwa wakitakiwa kutaja kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara.

Baada ya kubaini kuwa bajeti ya halmashauri hiyo ni karibu Sh29 bilioni ikijumuisha mapato ya ndani na ruzuku kutoka Serikali Kuu, Rais Magufuli aliwaagiza viongozi hao kupitia baraza la madiwani kufanya marekebisho yatakayowezesha kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami.

Akihutubia wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma mbalimbali za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Rais Magufuli alitoa wiki moja kuanzia juzi kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kutia saini makubaliano ya mkataba wa ujenzi wa Daraja la Kigongo - Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2.

Daraja hilo litakalokuwa refu kuliko yote Afrika Mashari na Kati linaunganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema na linajengwa kupita juu ya Ziwa Victoria kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni zinazotokana na mapato ya ndani.

“Kila siku watu wamekuwa wakisubiri feri (kwa muda mrefu) ... haiwezekani kila siku tunategemea feri. Unafika pale mama mjamzito mpaka ukasubiri feri; uchungu utakusubiri wakati mtoto anataka atoke? Pale wameshakufa watu. Tumeomba fedha (kutoka kwa wafadhili) tumekosa. Tumeamua tunajenga kwa fedha zetu wenyewe,” alisema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo pia aliagiza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoa Sh2.2 bilioni na Manispaa ya Ilemela Sh1.8 na kufikisha jumla Sh4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliagizwa kutafiti kwa nini wagonjwa wengi wa kansa wanatoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Rais Magufuli pia alizungumzia suala la bei ya pambana na kusisitiza kuwa bei elekezi ya zao hilo kuu katika Kanda ya Ziwa ni Sh1, 200 kwa kilo.

Mradi wa chelezo, meli mpya

Rais Magufuli pia aliagiza mradi wa ujenzi wa chelezo, meli mpya na ukarabati wa Mv Victoria na Mv Butiama kukamilika ifikapo Machi 31, 2021 kwa mujibu wa mkataba.

Mei 20 mwaka huu, Hamissi aliwaambia wanahabari kwamba ujenzi wa chelezo na meli mpya katika Bandari ya Mwanza Kusini, ulikuwa umekamilika kwa asilimia 30.

Alisema ujenzi wa meli hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo kati ya Bandari ya Mwanza na Bukoba ulikuwa umekamilika katika hatua ya michoro, kuagiza vifaa na ukataji wa vyuma.

Gereza la Butimba

Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, akiwa katika Gereza Kuu la Butimba, alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro kukaa na maofisa wake wa idara ya upelelezi kukamilisha upelelezi wa kesi za mahabusu zaidi ya 900 wanaosota gerezani kwa kukosa dhamana.

“Muangalie kesi za kubambikia na zisizo na mashiko na kuharakisha upelelezi ili hawa (mahabusu) waliocheleweshewa (kesi zao) wapate haki zao (ya kufungwa au kuachiwa huru),” aliagiza Rais Magufuli huku akishangiliwa na mahabusu na wafungwa.

Awali, mfungwa Karikina Nyamboge alimshtaki ofisa usalama wa gereza hilo aliyemtaja kwa jina moja la Mwasifiga kwa kunyanyasa wafungwa na Rais kumwagiza kuwa rafiki na mfungwa aliyemtaja huku akimuonya kutomwekea kinyongo.

Rais pia aliwaagiza wakuu wa Magereza nchini kubuni mikakati ya kuingiza kipato kitakachosaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizo ndani ya uwezo wao huku akiahidi kutoa magari mawili na trekta kwa gereza hilo la Butimba.

Pia, aliwapa wafungwa, mahabusu na askari wa gereza hilo ng’ombe watatu na magunia 15 ya mchele.

imeandikwa na Peter Saramba, Johari Shani na Jesse Mikofu.