Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi SADC

Wednesday August 14 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), limetoa mapendekezo lugha ya Kiswahili kuanza kutumika kama lugha ya nne katika nchi 16 wanachama.

Katika lugha ambazo zinatumika mpaka sasa katika nchi 16 wanachama ni pamoja na Kiingereza, Kireno na Kifaransa.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Agosti 14, 2019 na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na baraza hilo.

Profesa Kabudi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania amesema baraza hilo halitoi uamuzi bali linatoa mapendekezo ambayo yanapelekwa kwa wakuu wa nchi wanachama kwa ajili ya kuyatolea uamuzi.

“Kwa sisi Watanzania itakuwa ni jambo la furaha na shukrani  kupendekeza kwa wakuu wa nchi  wakubali Kiswahili iwe lugha ya nne rasmi kutumika katika nchi 16 za SADC na kwa kuanzia itumike katika ngazi ya baraza la mawaziri na itumike katika kutoa hotuba au kuongea na siku za usoni itumike katika kutoa tafsiri za nyaraka.”

“Kwetu ni heshima kubwa kwa kuwa Kiswahili ambacho ni lugha ya ukombozi, sasa lugha yetu itaafikiwa kama lugha ya nne rasmi ya jumuiya yetu kama wakuu wa nchi wataafiki,” amesema Profesa Kabudi.

Advertisement

Advertisement