Kitilya, wenzake wapandishwa upya kizimbani, wasomewa mashtaka 58

Muktasari:

Aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne Shose  Sinare, Sioi  Solomon pamoja na washtakiwa wapya Bedason Shallanda na Alfred Misana wamepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka 58


Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka mapya 58, yakiwemo ya utakatishaji wa fedha na kujihusisha na mtandao wa uhalifu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Hashimu Ngole akisaidia na Pendo Makondo na Patrick Mwita, amedai leo Ijumaa Januari 11, 2019, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka hayo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2019.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine ni Shose Sinare, Sioi Solomon pamoja na wengine wapya waliounganishwa katika kesi hiyo, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Kabla ya kusomewa mashtaka hayo mapya 58, washtakiwa Kitilya, Sinare na Solomoni walifutiwa kesi yao ya zamani iliyokuwa na mashtaka manane chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai  ( CPA), sura ya 20  iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Walifutiwa mashtaka hayo, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza Mahakama hiyo kuwa hawana nia ya kuendelea na shauri hilo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri mahakamani kuhusu kesi hii