Kitilya,wenzake wajibu mashtaka yanayowakabili

Muktasari:

  • Kamishna Mkuu mstaafu wa TRA na wenzake wanne wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Ufisadi, leo wamejibu mashtaka yanayowakabili, baada ya kesi hiyo kuingia katika hatua ya usikilizwaji wa awali

Dar es Salaam. Hatimaye Kamishna Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wamejibu mashtaka yanayowakabili. 

Washtakiwa hao wamejibu mashtaka hayo, leo Jumatano Machi 13, 2019, katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama  ‘Mahakama ya Mafisadi’, wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo, ikiwa ni mara ya kwanza tangu waliposhitakiwa kwa makossa hayo.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2019, ni Miss Tanzania wa mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon ambao walikuwa maafisa wa Benki ya Stanbic.

Wengine ni aliyekuwa Kamishna wa Sera na Madeni Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda (kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana, ambaye alikuwa Kamishna Msaidizi wa Sera na Madeni kutoka wizara hiyo ambaye kwa sasa yuko wizara ya afya.

Katika hatua ya usikilizwaji wa awali kwanza husomewa upya mashtaka yanayowakabili na kisha wanatakiwa kujibu ama kwa kukubali au kukana makosa hayo na baada ya hapo upande wa mashtaka huwasomea washtakiwa maelezo ya kesi inayowakabili.

Kitilya na wenzake kabla ya kusomewa maelezo ya awali wamekumbushwa kwanza kwa kusomewa upya mashtaka na wakatakiwa kujibu kama wanakubali au wanakataa.

Washtakiwa hao wamesomewa shtaka moja moja na kuulizwa mmoja baada ya mwingine iwapo anakubaliana na shtaka hilo au la. Hata hivyo, washtakiwa wote wamekana mashtaka yote.

Baada ya hatua hiyo Jaji Sirilius Matupa anayesikiliza kesi hiyo ameiahirisha kwa muda ili kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kuandaa nakala za kutosha za maelezo ya kesi kwa ajili ya mawakili na washtakiwa ili waweze kuwa wanafuatilia wakati upande wa mashtaka unawasomea washtakiwa hao maelezo ya kesi.

Hivi sasa pande zote , upande wa mashtaka na utetezi wakiwemo washtakiwa wanasubiri muda ufikie ili waingie ndani tayari kwa kuanza kusoma maelezo ya kesi na kisha kuendelea na hatua nyingine zinazofuata.

Kitilya na wenzake wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 58 na mashtaka 49 ni ya utakatishaji fedha, matatu ya kughushi na mawili ya kutoa nyaraka za uwongo.

Mashtaka mengine, moja la kuongoza mtandao wa uhalifu, shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, moja lingine la kula njama za kutenda kosa kwa nia ya kumdanganya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi.

Makosa hayo yalitokana na mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingireza, kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4, kupitia kampuni ya Egma T Ltd.

Katika mashtaka hayo wanadaiwa kujipatia Dola za Marekani 6 milioni kwa njia za udanganyifu kupitia kampuni ya Enterprises Growth Market Advisors (EGMA) kama ada ya uwezeshaji wa mkopo huo ya asilimia 2.4 na kisha kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Walipandishwa kizimbani mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Apri Mosi, 201 na kusomewa mashtaka manane yakiwemo ya utakatishaji fedha, lakini hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi kama hizo.

Baadaye Februari 12 walifutiwa mashtaka lakini wakakamatwa na kupandishwa tena kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka upya huku mara hii wakiongezewa mashtaka mengine kabla ya kuhamishiwa Mahakama ya Mafisadi kwa ajili ya usikilizwaji baada ya upelelezi kukamilika