VIDEO: Kitwanga aeleza kushtushwa taarifa za kifo

Mbunge wa jimbo la Misungwi,  Charles Kitwanga,  Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake katika kijiji cha Usagara  jana baada ya kurejea kutoka nchini India alikokuwa amelazwa kwa matibabu. Picha na Ngollo John

Muktasari:

  • Mei 21, 2016 Rais Magufuli alimfuta kazi Kitwanga kutokana na sababu iliyotajwa alibainika kuingia bungeni akiwa amelewa.

Misungwi. Mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza, Charles Kitwanga aliyejerea nchini akitokea kwenye matibabu India amewananga waliomzushia kifo akisema “ni mzima wa afya tele”.

Kitwanga, waziri wa kwanza wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Awamu ya Tano alikuwa mgonjwa kwa muda na amerejea baada kutibiwa nje ya nchi.

“Namshukuru Mungu nina afya njema, nimewasamehe walionizushia kifo,” alisema Kitwanga akiwa nyumbani kwake Usagara wilayani hapa jana.

Alisema akiwa India alipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu watu kumzushia kifo jambo alilosema lilimsononesha.

Kitwanga alianza kuumwa Januari 30, 2019 akiwa bungeni jijini Dodoma alikotibiwa na kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili kabla ya kupewa rufaa kwenda India kwa matibabu zaidi.

Februari 2, Rais John Magufuli alimtembelea Muhimbili na kumjulia hali na mkuu wa idara ya magonjwa ya dharura wa hospitali, Dk Juma Mfinanga alimweleza Rais kuwa hali ya Kitwanga ilikuwa inaendelea vizuri ikilinganishwa na alipofikishwa kutoka jijini Dodoma.

Akiwa wodini hapo, Rais Magufuli alishiriki sala ya kumuombea mbunge huyo na kuwashukuru madaktari na wauguzi kwa juhudi walizozifanya kuwahudumia wagonjwa.

Mei 21, 2016 Rais Magufuli alimfuta kazi Kitwanga kutokana na sababu iliyotajwa alibainika kuingia bungeni akiwa amelewa.

Kabla ya kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kitwanga ambaye ni mbunge wa Misungwi kwa awamu ya pili sasa, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kisha Naibu Waziri wa Mawasiliano na Sayansi katika Serikali ya Awamu ya Nne.