Kitwanga aitwanga wizara ya maji, asema yasije kujitokeza ya IPTL na Lugumi

Monday June 24 2019

 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ametoa tahadhari kwa Serikali ya Tanzania kuwa katika Wizara ya Maji kuna mhandisi mshauri anayefanya mambo ya ovyo na huenda akasababisha hali ya sintofahamu kama ilivyotokea katika wizara nyingine miaka ya nyuma.

Amesema yanayofanyika yanatakiwa kutazamwa vyema ili kutolipeleka Taifa katika mgogoro kama ilivyokuwa kwa kampuni ya Lugumi Enterprises na za kufua umeme za  Symbion na IPTL.

Kampuni ya Lugumi ilitajwa kushindwa kukamilisha ufungaji wa mashine za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi.

Tangu mwaka 2013 hadi 2016 Serikali ya Tanzania kupitia Bunge ilikuwa imetekwa na mvutano kuhusu uhalali wa kuchotwa Sh320 bilioni kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Akaunti hiyo ilianzishwa kumaliza mgogoro wa malipo kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Kampuni ya kuzalisha umeme ya Symbion kwa nyakati tofauti imewahi kuingia katika mzozo na Tanesco kuhusu ukiukwaji wa mikataba ya uzalishaji wa nishati hiyo.

Mbunge huyo Misungwi (CCM) ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 24, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali ya Tanzania mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Advertisement

“Pale Wizara ya Maji kuna matatizo maana tangu Serikali ya Awamu ya Nne tulikuwa na mradi wa kutoa maji Ruvu kwenda Kimara, mradi wa Ukerewe, sasa hivi tuna mradi wa kutoa maji Shinyanga kwenda Nzega, Igunga na  Tabora na mradi wa wilaya 29 ambao una matatizo.”

“Pale (wizarani) kuna mhandisi mshauri ambaye kwa miradi yote niliyoisema ameshiriki, kushiriki kwake hakuna tija sana kwenye nchi yetu. Naibu Spika (Dk Tulia Ackson) nitakuletea rundo la makaratasi uipelekee Serikali ijue Watanzania wanajua, wanaelewa nini kinachoendelea,” amesema Kitwanga.

Amesema alifikia hatua ya kuzisaka ofisi za mhandisi huyo mshauri lakini alipozibaini zilipo alishangaa.

“Ukiona mahala ofisi zake zilipo ndipo hapo naibu spika itabidi ofisi yako iwasiliane na Serikali hatutakuwa na muda tena wa kuona yanatokea yale wakati wa Symbion, Lugumi, IPTL na haya yatakuwa mabaya zaidi kwa jinsi nilivyoona na nilivyosoma,” amesema Kitwanga.

Ametaka Serikali kupewa taarifa kwamba mambo si mazuri, “Tuna umeme na tuna nguvu kazi tutawezaje kuwa na viwanda vinavyoweza kufanya kazi kama havipatiwi maji, maji yanahitajika sana katika uendeshaji wa viwanda”

Advertisement