Matokeo kidato cha IV: Shule za Serikali, Seminari, vipaji maalumu zaporomoka

Saturday February 14 2015

Katibu Mtendaji wa  baraza la Taifa la

Katibu Mtendaji wa  baraza la Taifa la Mitihani, Dk. Charles Msonde akitangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa Kidato cha nne, yaliyotangazwa leo jijini Dar es Salaam .Picha na Said Khamis 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi

Dar es Salaam. Idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezea kwa asilimia 10.8 huku shule za serikali za vipaji maalumu, kongwe na seminari  zikiendelea kuporomoka na mwanafunzi wa kike kutoka Shule ya Sekondari ya Baobab mkoani Pwani, Nyakaho Marungu akiongoza Kitaifa. 

Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa Wastani wa Pointi (GPA) ambao yanaonyesha shule 10 bora kitaifa zote ni binafsi huku mkoa wa Tanga ukitoa shule tano kati ya kumi za mwisho.

Shule za vipaji kama za Ilboru, Mzumbe, Msalato, Kilakala, Tabora Boys, Kibaha na Tabora Girls na Shule kongwe zinazomilikiwa na Serikali za Pugu, Zanaki, Bwiru Boys, Minaki, Azania na Jangwani kwa miaka ya hivi karibuni zimekuwa hazifui dafu mbele ya vipaji vingine kutoka shule binafsi.

Katika matokeo hayo ya Shule ya Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera imeongoza Kitaifa ambapo mwaka jana alikuwa ya kwanza kwa shule zenye watahiniwa chini ya 40.

Akitangaza matokeo hayo leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde amesema waliofaulu mtihani huo ni 196,805 sawa na asilimia 68.33 ya 288,247 ya waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 235,227 sawa na asilimia 58.25 waliofaulu 2013.

Dk Msonde alisema wavulana waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61.

Advertisement

Katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) upande wa  sekta ya elimu ya Sekondari inaonyesha kwamba kiwango cha ufaulu mwaka huu kifikie asilimia 70 na mwakani asilimia 80 hata hivyo, Dk Msonde alisema: “tumejitahidi kwani ni asilimia kama moja na ushee ilibaki, walimu walifanya kazi nzuri na nina imani tutaifikia.”

Amesema watahiniwa 297,365 waliandikishwa kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana 139,400 sawa na asilimia 46.88 na wavulana 157965 sawa na asilimia 53.12. Watahiniwa wa shule walikuwa 244,902 ikilinganishwa na watahiniwa 367,163 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka 2013.

Advertisement