Kiwango cha umasikini Tanzania chapungua kwa asilimia mbili

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Jumamosi amezindua jengo la Takwimu na Ripoti ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya kaya binafsi Tanzania Bara ambayo imebaini kuwa kiwango cha umasikini umepungua.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kiwango cha umasikini wa mahitaji ya msingi kimepungua kwa asilimia 13 ndani ya miaka 26.

Majaliwa amesema hayo leo Jumamosi Juni 29, 2019 wakati akizindua jengo la ofisi ya Takwimu jijini Dodoma na Ripoti ya Matokeo ya Viashiria muhimu vya utafiti wa Mapato na Matumizi Binafsi kwa Tanzania Bara wa mwaka 2017/18.

Amesema mwaka 1991/92 kiwango cha umasikini wa mahitaji ya msingi kilikuwa asilimia 39.0.

"Hii ini dhahiri kuwa kuendelea kupungua kwa kiwango cha umasikini kunahitaji juhudi na maarifa ya ziada," amesema Majaliwa

Awali, Naibu Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Ashatu Kijaji amesema kiwango cha umasikini nchini kimepungua kwa asilimia  mbili ndani ya miaka mitatu.

Dk Kijaji amesema pia umasikini kwa watu waishio vijijini umepungua kwa asilimia 3.1 kati ya mwaka 2011/11 na 2017/18.

Amesema Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015 kiwango cha umasikini ilikuwa ni asilimia 28.2 lakini kwa miaka mitatu umepungua hadi asilimia 26.4.