Klabu yapinga kupokonywa pointi tisa kwa kumtumia kipa Mnigeria bila cheti halali

Muktasari:

Kipa huyo aliichezea timu ya taifa ya Nigeria kwenye fainali zilizopita za Kombe la Dunia nchini Russia na ndio kwanza alikuwa amehamia Cuprus kwa mkopo akitokea Deportivo la Coruna ya Hispania

 


Klabu ya daraja la kwanza nchini Cyprus imekata rufaa kupinga kupokonywa pointi tisa kutokana na matukio ya nje ya uwanja, yakimuhusisha kipa wa kimataifa wa Nigeria, Francis Uzoho ambaye ndio kwanza amesajiliwa.

Chama cha Soka cha Cyprus jana kilifuta matokeo ya ushindi wa Anorthosis Famagusta wa bao 1-0 dhidi ya Apollon Limaasol ambayo sasa imepewa ushindi wa mabao 3-0 kutokana na Uzoho kucheza akiwa na cheti cha vipimo vya afya ambacho si halali.

Anorthosis pia ilipata pigo jingine kutokana na kupokonywa pointi sita na hivyo kufikia jumla ya pointi tisaa.

Uzoho, 20, ambaye aliidakia Nigeria katika fainali zilizopita za Kombe la Dunia, Oktoba mwaka juzi alikuwa kipa wa kwanza mdogo kutoka nje kwenye Ligi Kuu ya Hispania baada ya kucheza mechi yake ya kwanza na Deportivo La Coruna akiwa na umri wa miaka 18.

Daktari wa Anorthosis, Kyriacos Yiangou ni mmoja wa watu watatu waliokamatwa na baadaye kuachiwa na polisi kutokana na sakata hilo la cheti cha vipimo vya afya cha Uzoho, ambaye alisajiliwa kwa mkopo kutoka Deportivo mapema mwaka huu.

Cheti hicho kilitolewa kinyume na sheria. Kilitolewa wakati mchezaji huyo akiwa kwenye ndege kuelekea Cyprus, siku moja kabla ya Februari 2, siku ya mechi dhidi ya Apollon.

Apollon ililalamika kuwa Uzoho aliwasili kwenye kisiwa hicho kilicho Bahari ya Mediterranean muda mfupi kabla ya saa 8:00 Ijumaa ya Februari mosi, na bado ofisi ya taifa ya michezo inayohusika na utoaji wa vyeti hivyo ilifungwa saa 6:30. 

Uzoho amefungiwa kucheza mechi moja na amepigwa faini ya dola 1,130 (sawa na zaidi ya Sh2 milioni za Tanzania.

Kupokonywa pointi hizo kunatakiwa kuanze rasmi siku nane baada ya uamuzi huo wa Jumatatu, kitu ambacho kitaifanya Apollon kupanda juu ya wapinzani wao, APOEL Nicosia na kushika usukani wa ligi ya Cyprus kabla ya timu hizo kukutana Jumapili inayofuata.