Kodi ya mkaa itahamasisha matumizi ya nishati salama

Mjasiriamali na mvumbuzi wa mashine ya mkaa, Iddi Nyachenga akitoa mada katika mjadala wa Jukwaa la Frika lililojadili matumizi ya mkaa, uchumi na mazingira yetu, jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Mkurugenzi wa Masoko wa ORYX, Mohammed Mohammed. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dar es Salaam. Je unaijua sifa ya gesi au umeme kwa afya yako pindi unapofanya matumizi ya nishati hizo kwa ajili ya kupikia vyakula mbalimbali kwenye maisha yako ya kila siku.

Ukitumia nishati ya gesi au umeme ni nadra kuona moshi katika jiko lako tofauti na kuni na mkaa wa kawaida unaotokana na misitu.

Je umewahi kujiuliza ni vipi unaweza kupata nishati nyingine yenye gharama nafuu isiyokuwa na moshi au madhara ya kiafya kwa binadamu ambayo wengi huitaja kuwa ni nishati salama na rafiki kwa mazingira?

Hiki ni kilio ambacho watu wengi hutamani kupata mtetezi kwa kuwa na nishati salama na gharama nafuu tofauti na mkaa au kuni hasa kwa kuwa gesi imejengewa dhana kuwa ni nishati ya gharama kubwa.

Kutokana na hali hiyo mtengenezaji wa mashine na mzalishaji wa mkaa mbadala, Idriss Hamis Nyachenga ameamua kutengeneza mkaa salama kwa mazingira, usioharibu misitu ambao umekuwa ukitumia malighafi mbalimbali ikiwamo vumbi la mbao kupata nishati hiyo.

Watengenezaji mbalimbali wa mkaa mbadala wanadai kuwa nishati hiyo ni bora na humfanya mtumiaji kulinda afya yake kwa kuwa inatengenezwa kwa kuzingatia viwango vya moshi tofauti na ule unaotokana na miti.

Wengi wanapendelea zaidi kutumia mkaa wa kawaida bila kujua madhara yake, lakini kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, watu 22,000 hufariki dunia nchini kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya mkaa wa kawaida na kuni.

Makamba ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli, anasema moshi unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni ni sawa na kuvuta pakiti mbili za sigara.

“Gharama za kiafya kutokana na uharibifu wa hewa unaotokana na mapishi ya kuni na mkaa ni dola 1.8 milioni za Marekani kwa mwaka. Jukwaa hili litatupeleka kwenye uelewa mmoja kuhusu jambo hili na hatua za kuchukua ili jamii na Serikali tuweze kuchukua hatua,” anasema Makamba.

Makamba alitoa kauli hiyo katika mdahalo wa Jukwaa la Fikra la Mwananchi lililofanyika Februari 7 na kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa Serikali, taasisi, kampuni na wananchi kutafuta suluhisho la pamoja kuhusu mkaa, nishati na mazingira. Jukwaa hilo lilifanyika katika ukumbi wa Kisenga, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Mjadala huo wa tatu tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo mwaka jana, uliandaliwa kwa pamoja na Mwananchi Communications Limited (MCL), ITV na Radio One ukiwa na mada ‘Mkaa, Uchumi na Mazingira Yetu’ na mgeni rasmi alikuwa Makamba.

Katika mdahalo huo, Nyachenga aliyekuwa mmoja wa wazungumzaji katika meza kuu anasema kwamba mbali na kutengeneza mashine pia anazalisha mkaa mbadala kwa kutumia malighafi za taka ngumu zikiwamo pumba na maganda ya karanga,

Nyachenga maarufu kama ‘Mkaa wa Idriss’ anasema kwamba matumizi ya mkaa mbadala yameleta mabadiliko ya kiteknolojia ambayo Tanzania imechelewa kuyafikia.

“Mkaa mbadala umeleta utofauti kati yake na ule utokanao na miti ambao umekuwa ukisababisha uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini. Nishati hii mbadala ni bora kwa kuwa maandalizi yake yanajali afya ya binadamu,” anasema Nyachenga.

Anasema kwamba kinachowakwamisha kufika mbali katika jitihada zao ni mamlaka husika kuwa bado hazijaweza kupambana vyema na mkaa unaotokana na miti ambao si rafiki kwa mazingira.

Pia, Nyachenga ameiomba Serikali kuangalia suala la ushuru katika mkaa mbadala kwa kuwa wamekuwa mstari wa mbele kulisaidia Taifa kwa kuajiri vijana kulinda na kuhifadhi mazingira.

“Wenzetu wanaozalisha mkaa wa miti hawalipi ushuru na wanaingiza fedha nyingi, lakini tunaozalisha mkaa mbadala tunalipia ingawa tunaingiza fedha kidogo,” anasema Nyachenga.

Anasema ni vyema Serikali ikatunga sheria itakayoelekeza taasisi yenye watu kuanzia 500 kuacha matumizi ya mkaa wa miti badala yake, waanze kutumia mkaa mbadala.

Naye mkurugenzi wa kampuni ya Mkaa Endelevu ambayo pia inatengeneza mkaa mbadala, Benjamin Lane anasema endapo mkaa wa miti utawekewa utaratibu wa kulipa kodi, bei itapanda na watumiaji watahamia katika nishati mbadala.

Lane pia anaongeza kwa kusema kwamba endapo Serikali itapunguza kodi katika mkaa mbadala hali hiyo itawaletea unafuu wananchi kutumia kwa wingi nishati hiyo badala ya mkaa wa kuni ambao unaharibu misitu na mazingira kwa ujumla.

Akichangia mjadala huo, mtafiti wa misitu Edward Maduhu anasema kwamba namna pekee ya kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana miti ni kujengwa kwa viwanda vingi vya kutengeneza mkaa mbadala.

“Kama tumeweza kutengeneza meza kwa mbao mbadala, basi hata katika mkaa mbadala tutaweza kumaliza hili tatizo. Kikubwa ni kukazana katika kujenga viwanda vya mkaa mbadala.

“Tanzania inatumia mbao asilimia 35, iliyobaki inatupwa, ikitumika yote kwa asilimia 100 hiyo iliyobaki na kutupwa itatengeneza mkaa mbadala,” anasema Maduhu.

Mchangiaji mwingine katika mdahalo huo, Dk Donati Ulomi anasema kwamba ni vyema Serikali ikahakikisha inawajengea vijana uwezo wa kuzalisha mkaa mbadala na hakuna haja ya kuogopa kwani mkaa wa kawaida utapotea taratibu.

“Serikali ifungue soko la mkaa mbadala na iwekeze kwa kutangaza kuwepo kwa nishati mbadala ili watu wengi waitumie,” anasema Dk Ulomi.

Naye Leonard Kushoka ambaye ni mzalishaji wa mkaa mbadala, akichangia mjadala huo anasema kwamba katika kampuni yake wametengeza mashine nyingi kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala ili kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na misitu.

“Miji iliyoendelea ndiyo inayotumia mkaa wa misitu kwa wingi. Ni vyema kuwekeza katika mashine ya kuzalisha mkaa mbadala ili kuwapa ajira vijana kwani malighafi zake ni rahisi kupatikana,” anasema Kushoka.