Kongamano kutoa elimu matumizi dawa za kulevya kufanyika Jumatano

Monday February 11 2019

By Bakari Kiango,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), imeandaa kongamano  kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu matumizi ya dawa za kulevya ambazo baadhi ya watu wakiwemo wasanii zimewaathiri.

Kongamano hilo, litafanyika Jumatano Februari 13, 2019  katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere na litafunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu Februari 11, 2019, Kamishna wa Tiba na Kinga wa DCEA , Dk Peter Mfisi amesema tatizo la dawa za kulevya ni kubwa na linawaathiri vijana wakiwemo wasanii wa fani mbalimbali.

"Tumeona ni vyema tukaitana na kujadiliana kwa kina kuhusu madhara ya dawa hizi. Tutawaambia ukweli washiriki wa kongamano hilo hali halisi ya dawa hizi," amesema Dk Mfisi.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Rogers Siyanga amesema wamejipanga kutoa elimu ya madhara kwa binadamu kwa kila dawa ya kulevya zikiwemo cocaine na heroine na kuwataka wasanii wahudhurie kwa wingi kongamano hilo kubwa.

" Njooni tuzungumze, tuelemishane kuhusu madhara ya dawa hizi. Tukiunganisha nguvu kwa pamoja tutaishinda vita hii," amesema Siyanga.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisso amesema kongamano hilo litawashirikisha washiriki takriban 1000 wakiwemo wasanii wa muziki, filamu, wachoraji na wasanifu," amesema Fisso.

Advertisement