Korosho zaiingizia Serikali zaidi ya Sh1 trilioni, lakini...

Dodoma. Licha ya kuiingizia Serikali zaidi ya Sh1 trilioni Januari pekee, malipo ya wakulima wa korosho yameendelea kusuasua.

Aidha, Serikali iko mbioni kuuza tani 200 za korosho nje ya nchi huku kukiwa na shehena ya kubwa iliyohifadhiwa kwenye maghala ambayo bado haijalipiwa.

Hayo yameelezwa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba bungeni Dodoma na kubainisha kuwa hadi sasa Serikali imelipa asilimia 59 ya fedha za wakulima wanaostahili baada ya kuuza korosho zao.

“Korosho ni zao lenye tija kwa Taifa na huliingizia fedha nyingi za kigeni. Kwa kipindi cha Januari 2018, limeingiza (zaidi ya) Sh1.13 trilioni ikilinganishwa na mazao mengine,” alisema Mgumba.

Katika ukusanyaji, alisema tani 213,000 zimeshapokewa ingawa zilizohakikiwa hadi sasa ni tani 129,000 na malipo kuanza kufanywa. Endapo tani zote 275,000 zinazotarajiwa kuvunwa mwaka huu zitapatikana, Serikali itatumia Sh907.5 bilioni kuwalipa wakulima kwa bei ya Sh3,300 kwa kila kilo.

Kuchelewa kwa malipo ya wakulima hao kumewaibua baadhi ya wabunge waliotaka majibu ya Serikali kuhusu hali hiyo. waliosimama na kuuliza jana ni Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftah Nachuma, Hawa Ghasia wa Mtwara Vijijini (CCM) na Nape Nnauye wa Mtama (CCM).

Nachuma alihoji ni kwa nini Serikali inasuasua katika malipo ya wakulima na kuitaka kueleza kama ipo tayari kuondoa changamoto zilizopo katika zao la korosho ili liweze kuleta tija.

Alizitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni pamoja na madai ya kuwapo kwa vitendo vya rushwa kwa maofisa waliopo mikoa ya Kusini.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea mikoa hiyo kujionea mwenendo wa ulipaji alionyesha hofu kuwa mchakato wa malipo umegubikwa na rushwa.

Nape alikazia hofu ya Waziri Mkuu kwa kuhoji ni hatua gani zimechukuliwa kwa watumishi husika ili kuifanyia kazi kauli ya Majaliwa.

Akijibu swali la Nape, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema wizara imeshachukua hatua kwa kuwasimamisha watumishi wanne ambao wakati wowote utaratibu ukikamilika watapelekwa mahakamani na akaitaka Ofisi ya Rais Tamisemi kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi walio chini yao.

Licha ya malipo ya wakulima, halmashauri pia hazipati stahiki zake kwa wakati kama ilivyotarajiwa. Ghasia alihoji inakuwaje Serikali iliyochukua jukumu la kununua korosho hailipi fedha kwa halmashauri ambazo ni muhimu katika kwa maendeleo.

Kuhusu kuzilipa halmashauri, Mgumba alisema: “Hadi jana Sh4 bilioni zimelipwa kwa wasafirishaji.