Kortini kwa kughushi nyaraka malipo ya korosho

Wednesday May 15 2019

 

By Haika Kimaro, Mwananchi [email protected]

Mtwara. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mtwara imewafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu washtakiwa wawili kwa makosa ya rushwa, kughushi na utakatishaji fedha.

Washtakiwa hao ni Juma Mbeve ambaye ni katibu mkuu wa Chama cha Ushirika Napacho na Agusto Nziku mfanyakazi wa benki ya NMB Nanyumbu ambaye akaunti ya mtoto wake ilitumika kuingiza fedha hizo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuingiza jina la mtoto wa miaka mitano katika malipo ya korosho na kujipatia Sh5.6 milioni kinyume na sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Mei 15, 2019 Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Stephen Mafipa amesema Mbeve anatuhumiwa kwa makosa ya kughushi nyaraka.

Amedai kwa kufanya hivyo alimwezesha mshtakiwa mwenzake, Nziku kujipatia kiwango hicho cha fedha kupitia akaunti yenye jina la mtoto wake ambaye haruhusiwi kuuza korosho wala hakuuza.

“Mbeve anashtakiwa kwa kosa la utakatishaji wa fedha haramu kinyume na vifungu namba 12(c) na 13(a) vya sheria ya kuzuia utakatishaji fedha haramu namba 12 ya mwaka 2016,” amesema Mafipa.

Kuhusu Nziku, amesema anashtakiwa kwa kosa la kusaidia kutendeka kosa kinyume na kifungu cha 30 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Mafipa amesema jina la mtoto wa mfanyakazi huyo wa benki liliingizwa kwenye orodha ya malipo huku wakijua  hastahili kuuza korosho na hakuuza.

Advertisement