Kosa hela tujue ujinga wako

Sunday January 20 2019

 

Nani aliyekuwa anafahamu kwamba unaweza kuogea sabuni ya unga na ukatakata kama umetumia sabuni ya kuogea? Kisha ukapata vimafuta vya mgando vya ‘bebi kea’ na ukameremeta kama umepaka zile ‘losheni’ za kiume za kunukia.

Na kumbe aisee unaweza kung’arisha kiatu chako mwenyewe nyumbani kikang’aa kuliko ‘tunavyong’arishaga’ kwa mafundi viatu mjini.

Haya yote tumefunzwa na mwezi Januari. Hakika wanaosema mjini shule kuna uwezekano hawajawahi kukutana na huu mwezi huko walipokuwa. Huu mwezi ni shule, ni madrasa, ni mafundisho ya kipaimara na komunio, ni sekondari, ni chuo, ni chuo kikuu, ni jando na ni kambi ya mafunzo ya ‘kijeda’.

Yaani Januari yenyewe itakufundisha maisha, itakufundisha kuwa wachamungu, itakuelekeza mahesabu na kukupa mbinu za kijeshi za kuendelea kuwa hai – Asante Januari.

Tukiweka nukta kwenye habari za Januari umeshawahi kusikia msemo wa Waswahili unaosema pata hela tujue tabia zako? Kama bado basi ndiyo umeusikia na unamaanisha kwamba, wewe ulivyo una tabia zako chafu ambazo zinaishi ndani kwa ndani – ambazo kuziona ni hadi ziamshwe. Na kitu pekee kinachoweza kuziamsha ni wewe kukamata pesa.

Watu wengi wakiwa na hali mbaya kifedha, akina baba kabwela wanakuwa na tabia za malaika. Wana adabu, wanaheshimu watu wengine, wachamungu na nyingine na nyingine.

Lakini sasa wakikamata pesa, zile tabia zao za ndani kwa ndani ndiyo zinaamka sasa. Ndiyo hapo utakapogundua kumbe kuna watu wana matusi, wanadharau, wanapenda wanawake, walevi mbwa wale wanaoukunywa pombe za darubini anazozisemea Mheshimiwa Mwanri, Pombe za Darubini, unakunywa ukiwa Tabora lakini unajiona uko Dar es Salaam. Watu wakikamata pesa utagundua mengi.

Lakini hiyo ni uhamisho kutoka kutokuwa na pesa kwenda kuwa na pesa. Vipi kuhusu uhamisho wa kuwa na pesa kwenda kutokuwa na pesa? Huu Waswahili wana msemo unasema kosa hela tujue ujinga wako.

Ujinga ni kufikiria kwamba marafiki uliokutana nao baa, wakakupachika jina la Meneja kwa sababu ya kuwanunulia vyombo kila siku, wanaweza kukusaidia shida zako halisi kipindi ambacho huna kitu. Pombe wanaweza kukusaidia, lakini shida halisi ni chakula, kodi na mahitaji mengine muhimu ya familia yako nyumbani – hawatakusaidia.

Ujinga ni kudhani kuwa, sasa kwa sababu huna kitu, ndiyo mkeo ataanza kulipa kisasi kwa yale uliyokuwa unamfanyia wakati una hela; kurudi nyumbani usiku sana ukiwa mbwiii, kumdharau, kumtukana na kutomjali. Ndiyo anaweza kufanya, lakini kiini cha ujinga hapa ni kule kujihami, yaani hata mwanamke hajaanza kukunyoosha unavyostahili, wewe unaanza kulalamika ‘una dharau sasa hivi kwa sababu hela hakuna.’

Huo wote ni ujinga unaomezwa na hela ambazo labda uko nazo sasa hizi. Kwa hiyo kabla hujafika huko ni bora uchague moja kati ya kuacha tabia chafu zinazobabishwa na hela ili zikiisha usiumbuke, au kuhakikisha hela zako haziishi ili usije ukaishi kwenye ujinga wako.

Advertisement