Kuachiwa huru kwa Gbagbo kunafungua ukurasa mpya Ivory Coast

Muktasari:

Macho na masikio ya wengi yaliekelezwa nchini humo kutokana na mvutano mkali wa kisiasa uliokuwapo wakati Rais wa wakati huo aliyekuwa akitetea kiti chake katika uchaguzi huo, Laurent Gbagbo, alipokuwa akikabana koo na mpinzani wake, Alassane Ouattara.

Moja ya matukio makubwa ya kisiasa barani Afrika mwaka 2010 ilikuwa ni uchaguzi mkuu wa Ivory Coast ambapo jumuiya ya kimataifa ilitega sikio kwa taifa hilo mashuhuri zaidi kwa kilimo cha kakao duniani.

Macho na masikio ya wengi yaliekelezwa nchini humo kutokana na mvutano mkali wa kisiasa uliokuwapo wakati Rais wa wakati huo aliyekuwa akitetea kiti chake katika uchaguzi huo, Laurent Gbagbo, alipokuwa akikabana koo na mpinzani wake, Alassane Ouattara.

Hadithi ya uchaguzi huo ilikuwa hivi; awali ulipaswa kufanyika mwaka 2005, lakini ilishindikana kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha hali ngumu ya kuuratibu.

Baada ya hapo uliahirishwa mara kwa mara na hatimaye Machi 4, mwaka 2007, Serikali na waasi wa kikundi cha New Forces walitia saini mkataba wa kuacha mapigano ambapo baadaye ikatangazwa uchaguzi huo utafanyika Novemba 29, 2009.

Hata hivyo, Novemba 11, mwaka huo ilitangazwa kupanguliwa tena kwa uchaguzi huo na kuelezwa kuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa Februari, 2010, haukufanyika katika tarehe hiyo badala yake wananchi walisubiri hadi Desemba mwaka huo.

Uchaguzi huo uligubikwa na mvutano mkali ambapo Gbagbo aliyekuwa na wafuasi wengi upande wa Kusini mwa Ivory Coast huku mpinzani wake, mwanasiasa wa siku nyingi wa upinzani Ouattara ambaye sasa ni Rais wa nchi hiyo, alikuwa akionekana kuungwa mkono kwa wingi upande wa Kaskazini.

Desemba 2, 2010 Tume Huru ya Uchaguzi ya Ivory Coast (IEC) ilimtangaza Ouattara kuwa mshindi wa awamu ya pili ya uchaguzi huo baada ya kupata asilimia 54 ya kura zilizopigwa. Awali katika awamu ya kwanza ya uchaguzi huo Oktoba 2010, hakuna mgombea aliyepata wastani uliomruhusu kutangazwa mshindi moja kwa moja.

Kilichofuata ni Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo kutangaza kutoyatambua matokeo yaliyomtangaza Ouattara kuwa mshindi kwa madai kwamba yalikuwa batili ambapo siku iliyofuata ilimtangaza Gbagbo kuwa ndiye mshindi.

Baadaye kila mmoja akajitangaza mshindi na kujiapisha kushika wadhifa wa urais.

Hatua hiyo iliingiza Ivory Coast katika mgogoro mpya uliodumu kuanzia wakati huo hadi mwaka 2011 na kushuhudiwa watu 3,000 wakipoteza maisha huku wengine zaidi ya 500,000 wakiyakimbia makazi yao.

Jumuiya ya kimataifa ukiwamo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Marekani, Ufaransa, Jumuiya ya Kibiashara ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas), zote zilimuunga mkono Ouattara ambaye iliaminika amemshinda Gbagbo katika sanduku la kura na kumtaka kiongozi huyo kuachia madaraka kwa njia ya amani.

Gbagbo alikaidi shinikizo la kung’oka na kuitaka UN kuviondoa vikosi vyake vya waangalizi wa amani vilivyokuwa nchini humo lakini umoja huo ulipuuza agizo hilo.

Jumuia ya kimataifa ilizidi kumwandama Gbagbo ikimtaka aondoke madarakani. Aliwekewa vikwazo mbalimbali ikiwamo Benki ya Dunia kutangaza kusitisha mikopo kwa nchi hiyo huku kiongozi huyo na washirika wake wakipigwa marufuku kusafiri.

Aprili 11, 2012 Ouattara aliingia rasmi Ikulu kuanza kuiongoza nchi hiyo katika awamu yake ya kwanza huku Gbagbo akianza safari ya mashtaka mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC). Kutokana na vurugu zilifuata baada ya uchaguzi huo, Gbagbo aliwekwa kizuizini nyumbani kwake kwa miezi saba mjini Abidjan kabla ya kukamatwa na kusafirishwa mjini The Hague, Uholanzi iliko ICC. Gbagbo alikuwa kiongozi mkuu wa kwanza wa nchi wa zamani kupandishwa mbele ya ICC.

Mashtaka yake ICC

Mbele ya ICC, Gbagbo alishitakiwa kwa makosa dhidi ya ubinadamu, mauaji, ubakaji na utesaji yaliyotokana na vurugu za baada ya uchaguzi ambao Ouattara alishinda kwa asilimia 54 zilizotangazwa na tume ya uchaguzi. Hata hivyo Gbagbo alikana kuhusika na makosa hayo.

Katika uamuzi wao Jumanne wiki hii, majaji wa ICC walisema Gbagbo hana shitaka la kujibu na kuagiza aachiwe huru mara moja. Walisema wameshindwa kuhusisha madai ya mikakati ya kiongozi huyo kuendelea kusalia madarakani na makosa aliyoshitakiwa mbele ya ICC.

Jaji Cuno Tarfuser wa mahakama hiyo alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi unaothibitisha pasi na shaka kuwa hotuba za Gbagbo zilielekeza kutendeka kwa makosa yaliyosababisha madhara yaliyotokea. Hata hivyo, alisema upande wa mashitaka unayo haki ya kukata rufaa baada ya uamuzi huo kuwekwa katika maandishi.

Hukumu hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na kila upande kati ya wale wanaomuunga mkono kiongozi huyo na wanaompinga. “Nina furaha isiyo kifani. Hatimaye haki imetendeka,” anasema Gragbayou Yves, mfuasi wa Gbagbo aliyesafiri kutoka Ufaransa hadi The Hague kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo.

Wasiomuunga mkono Gbagbo wanahoji juu ya hali walizonazo sasa wanazodai zimetokana na vurugu hizo zinaweza kufidiwa kwa namna gani. “Kama Gbagbo ameachiwa huru tulioathiriwa na vurugu hatuwezi kupata haki,” anasema Karim Coulibaly, ambaye alipoteza mkono wake kutokana na vurugu hizo.

Kauli ya mke wake

Mara baada ya kutangazwa kuachiwa huru kwa Gbagbo, mke wake Simone Gbagbo akizungumza na Shirika la utangazaji la BBC alisema haki imetendeka.

“Ni uamuzi niliokuwa nikiusubiri kwa muda mrefu. Tangu awali nilijua kwamba Rais Gbagbo hana hatia juu ya kila kitu alichokuwa akituhumiwa kuhusika nacho,” anasema.

Simone alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani na makosa mbalimbali yaliyotokana na vurugu za baada ya uchaguzi huo.

Serikali ya Ivory Coast ilikataa kumkabidhi Simone kwa ICC ikisema itamshitaki na kumhukumu katika mahakama za ndani. Hata hivyo, Simone alinufaika na msamaha wa Rais Ouattara mwaka jana ambaye alisema ameamua kumsamehe ili kufungua milango ya maridhiano kwa mustakbali wa taifa hilo.

Ingawa bado haijafahamika msimamo wa Gbagbo baada ya kuachiwa huru, lakini wachambuzi wa siasa za nchi hiyo wanaelezea hatua ya kuachiwa huru kwa Simone inaweza kuwa dalili njema ya kurudi katika meza ya mazungumzo.

Imetayarishwa na Suleiman Jongo kwa msaada wa mitandao mbalimbali.