Kudharau chanjo kunavyoweza kuwa hatari kwa mama na mtoto

Licha ya ujauzito kuwa furaha, mmjamzito anaweza kupoteza maisha yake na ya mtoto anayetarajia kumzaa endapo hatofuata taratibu za kitabibu zinazotakiwa katika kukuza na kulea mimba.

Hata hivyo, mjamzito anaweza kupunguza hatari ya kupoteza maisha, ikiwa atahudhuria kliniki mara kwa mara ili kujua maendeleo yake.

Santiel Kinyongo, Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Morogoro anasema kuna umuhimu wa mjamzito kuzingatia na kupata chanjo zote za kumlinda mtoto wake pindi anapojifungua.

Anasema mjamzito pindi anapoanza kliniki, anatakiwa kupata chanjo ya pepopunda.

Kinyongo anasema pepopunda ni ugonjwa hatari unaoambukizwa na bakteria ambao huingia mwilini kupitia kwenye kidonda au jeraha.

Sehemu nyingi duniani, hasa katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, wajawazito hujifungua katika mazingira magumu (ikiwamo sehemu zisizo safi na salama) na hii humuweka mama na mtoto katika hatari ya kupata magonjwa, hasa pepopunda.

Kinyongo anasema watoto wachanga hufa kwa ugonjwa huo wanaoupata kama wajawazito hawakupata chanjo.

Kutokana na umuhimu wake, Kinyongo anasema mjamzito anatakiwa apate chanjo ya pili ya pepopunda baada ya miezi miwili na atarudia tena chanjo baada ya miezi sita. Chanjo ya nne na tano, atapewa baada ya mwaka mmoja.

Anasema kwa utaratibu huo, mama aliyepata chanjo zote hizi atakuwa amejikinga na pepopunda kwa miaka 20.

Tafiti zinaonyesha wanawake wengi katika nchi masikini hawapati chanjo kwa ajili yao na watoto wao kwa sababu mbalimbali, ikiwamo uhaba na umbali wa vituo vya afya.

Pia, baadhi ya wanawake huamini hakuna haja ya kwenda hospitali baada ya kujifungua salama.

Catherine Maganga, ambaye ni Ofisa Muuguzi (mtoa huduma za afya kwa mama na mtoto) anasema wajawazito 156 kati ya 100,000 hufariki mkoani Morogoro kutokana na kutopata chanjo kwa ajili yao na watoto wanaowazaa.

Anasema jukumu la chanjo siyo la mjamzito pekee, bali mzazi mwenza, ndugu, jamaa na marafiki wanapaswa kuhakikisha linazingatiwa wakati wote hata baada ya kujifungua.

Maganga anasema watoto walio chini ya miaka mitano wapo katika hatari ya kupata magonjwa kwa sababu kinga zao za mwili zipo chini ukilinganisha na watu wazima.

Anayataja baadhi ya magonjwa yanayokingwa nchini kupitia chanjo ni polio, pepopunda, kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, surua na nimonia.

Anasema chanjo kwa watoto wadogo inalenga kuzuia na kutokomeza kabisa magonjwa yaliyotajwa.

Maganga anasema chanjo ya DPT inamlida mtoto dhidi ya magonjwa mengi ikiwamo dondakoo, kifaduro, nimonia na homa ya ini, hivyo ni muhimu mtoto mchanga kupatiwa chanjo hiyo baada ya kuzaliwa.

Kwa upande wa chanjo ya Lota anasema inazuia kuharisha kwa mtoto mchanga na chanjo ya BCG inazuia kifua kikuu na hutolewa pindi mtoto anapozaliwa au kufika kliniki kwa mara ya kwanza.

Anasema chanjo hizi ni muhimu kwa mtoto kwa sababu magonjwa yake ni ya kuambukiza.

Maganga akitolea mfano, anasema kifua kikuu kinasababishwa na vimelea vya bakteria kwa njia ya hewa.

Anasema kwa watoto ambao kinga yao ipo chini, wanakuwa katika hatari kubwa kupata maambukizi ikiwa hawakupatiwa chanjo.

Kwa upande wa polio anasema ugonjwa huo husababishwa na virusi ambavyo huenezwa kwa kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi.

Ugonjwa huu huwapata watu wa rika zote, lakini watoto wadogo ndio waathirika zaidi na ni vizuri wakipatiwa chanjo zote nne kwa kufuata ratiba zake.

Maganga anasema kwa kuwa watoto wakati mwingine wanacheza katika mazingira hatarishi, chanjo ya pepopunda ni muhimu kwao kwa kuwa hupata majeraha na vidonda, hivyo vimelea vya ugonjwa huo vinaweza kuwaathiri ikiwa hawakupatiwa chanjo.

Ili kuhakikisha mjamzito na mtoto wanavuka salama baada ya uzazi, Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likihimiza huduma za afya ikiwamo chanjo kwa wajawazito na watoto.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya jitihaza kubwa kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kuhakikisha wajawazito na watoto wanavuka salama baada ya kujifungua.