Kumekucha Uchaguzi Mkuu 2015, Lowassa atikisa CCM, upinzani

Thursday November 13 2014

viongozi wa vyama na Serikali nchini Tanzania

viongozi wa vyama na Serikali nchini Tanzania ambao majina yao yanatajwa na  wananchi kuwa wanaweza kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu mwakani. 

By Goodluck Eliona, Mwananchi

Dar es Salaam. Kumekucha. Pengine hilo ndilo neno linalofaa kutumika kuelezea matokeo ya utafiti kuhusu kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 ambayo yanaonyesha kuwa iwapo ungefanyika leo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa angeibuka mshindi.

Wakati Lowassa angeibuka na ushindi kwa asilimia 13 na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda angefuatia kwa karibu akiwa na asilimia 12 huku Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akiwa wa tatu kwa asilimia kumi na moja.

Hata hivyo, asilimia 33 ya wananchi waliohojiwa walisema bado hawajaamua wampigie kura mgombea gani.

Utafiti huo wa Taasisi ya Twaweza unayoonyesha wagombea hao kukabana kwa tofauti ya asilimia mojamoja na ambao ulitangazwa Dar es Salaam jana, ulifanywa Septemba 2014 kwa kuwahoji wananchi 1,445 kutoka Tanzania Bara.

Akitangaza matokeo hayo, mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi alisema utafiti huo ni wa tatu kufanyika nchini na kwamba awamu ya kwanza ilifanyika mwaka 2012 na Lowassa alipata asilimia sita kabla ya mwaka jana na mwaka huu kuibuka na asilimia 13.

Akimzungumzia Pinda, mtafiti huyo alisema mwaka 2012 alipata 16, lakini zilishuka mwaka 2013 hadi kufikia asilimia kumi na moja na kupanda tena mwaka huu hadi 12.

Advertisement

“Kwa upande wa Dk Slaa, mwaka 2012 na 2013 alipata asilimia 19 lakini sasa ameshuka hadi asilimia kumi na moja,” alisema Mushi.

Wagombea wengine waliotajwa na asilimia zao kwenye mabano ni Profesa Ibrahim Lipumba (6%), Dk John Magufuli (3%), Freeman Mbowe (3%), Samuel Sitta (4%), Bernard Membe (5%) na Zitto Kabwe (1%).

“Hata hivyo, kitu muhimu cha kuangalia katika ripoti hii siyo tu majina ya mgombea, bali ni idadi ya wananchi asilimia 33 ambao wamesema hawajui watamchagua nani,” aliongeza Mushi.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa iwapo vyama vyote vya upinzani vitaungana na kumchagua mgombea urais mmoja, asilimia 41 ya wananchi waliohojiwa walisema wangemchagua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, akifuatiwa na Profesa Lipumba (14%), Mbowe (11%) na Zitto Kabwe (6%).

Wanasiasa wengine waliotajwa ni Tundu Lissu, Maalim Seif Sharif Hamad, James Mbatia na Augustino Mrema ambao kila mmoja aliambulia asilimia moja.

Wengi kuchagua CCM

Pia utafiti unaeleza kuwa iwapo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) utasimamisha mgombea mmoja wa urais dhidi ya CCM, asilimia 47 ya wananchi walisema wangeichagua CCM huku asilimia 28 wangempigia kura mgombea wa muungano wa upinzani. Asilimia 19 ya wananchi walisema watampigia kura mgombea bila kujali chama chake.

“Kura za kundi hili zitategemea ubora wa wagombea. Kama kura hizo zitagawanywa kwa CCM na upinzani, CCM itashinda urais kwa kuzidi upinzani kwa kura nyingi kiasi. Kutakuwa na kitisho kwa ushindi wa CCM endapo wapigakura wote watamchagua mtu badala ya chama watampigia mgombea wa upinzani, kitu ambacho kina uwezekano mdogo kutokea,” inasema ripoti hiyo.

Wananchi walia uchumi, afya na elimu

Wananchi walipoulizwa ni matatizo gani matatu makubwa yanayoikabili Tanzania walitaja ukosefu wa elimu bora, afya na hali mbaya ya kiuchumi na kwamba matatizo hayo yameshika nafasi ya juu kwa miaka mitatu mfululizo.

“Umaskini umeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka 2012 hadi 63 mwaka 2014, huku matatizo ya afya yakiongezeka kutoka asilimia 40 hadi 47 na elimu imeshuka kutoka asilimia 46 mwaka jana hadi 38 mwaka huu,” alisema Mushi.

Wabunge na ahadi zao

Katika utafiti huo, imeelezwa kuwa ahadi nyingi zilizotolewa na wabunge kwenye mikutano ya kampeni wakati wa uchaguzi hazijatekelezwa na kwamba asilimia 78 ya wananchi bado wanazikumbuka.

Ahadi nyingi zilizotolewa na wagombea zilihusu miradi ya ujenzi barabara, maji, ujenzi wa hospitali, kuboresha elimu, umeme, mikopo kwa vikundi, kuongeza ajira, kujenga madaraja na kuboresha kilimo.

Pia ripoti imeweka wazi kuwa karibu nusu ya wabunge wote huenda wasirudi tena katika nyadhifa zao. Asilimia 47 ya wananchi walioulizwa iwapo watampigia tena kura mbunge wao walisema hapana huku asilimia kama hiyo wakisema ndiyo.

Akizungumzia utafiti huo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu alihoji namna majina ya wagombea yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo yalivyopatikana huku akipendekeza namna sahihi ya kuwalinganisha wagombea hao.

“Walitakiwa kulinganishwa kwa mfano kwenye kilimo, watuambe Mizengo Pinda anaweza kufanya nini akilinganishwa na mgombea mwingine. Vinginevyo inakuwa ni mashindano ya urembo. Tunatumia muda mrefu kumchagua mbuzi Vingunguti kumbe atachinjwa kesho,” alisema Ulimwengu.

Kwa upande wake, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema hatashangaa kusikia kuna watu wengine wametoa ripoti nyingine kupinga utafiti huo kwa kuwa kumekuwapo na utamaduni wa kutokukubaliana na matokeo ya namna hiyo.

“Tafiti hupingwa na tafiti, kwa hiyo mtu asianze kupinga tu, fanya kama wao (Twaweza) jifunze kutumia takwimu,” alisema huku akionyesha kukasirishwa na watu waliokuwa wakitoa maoni ya kupinga ripoti hiyo.

Kauli ya Nape

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema anakubaliana na matokeo hayo kwa kuwa yamepatikana na njia ya simu katika nchi ambayo ina watumiaji wengi wa aina hiyo ya mawasiliano.

Hata hivyo, alisema: “Tatizo ahadi nyingi zinazotolewa na viongozi kwa wananchi hazitekelezwi. Tunasema asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima lakini asilimia mbili ya viongozi ndiyo walioahidi kuhusu kilimo.”

Mjumbe wa lililokuwa Bunge la Katiba, Maria Sarungi alisema ripoti hiyo haina habari njema kwa vyama vya siasa kwa sababu inaonyesha kuwa wananchi wamekosa imani ya kupata msaada, badala yake wameanza kumtafuta ‘mkombozi’ atakayewasaidia.

“Inapotokea asimilia 41 wanasema hawajui watamchagua nani huku asilimia 10 wakisema inategemea na mtu atakayejitokeza inaonyesha wananchi wanamtafuta mtu atakayewasaidia na siyo chama.

“Mambo ya wananchi yanatatuliwa na Katiba, tatizo la utawala bora na umaskini haliletwi na vyama vya siasa linaletwa na Katiba.”

Advertisement