Kuna msuli wa mwanamume na mwanamke

Mwanaume anacheza soka, kadhalika mwanamke anacheza, lakini watalaamu mbalimbali wa soka duniani, wamechambua ukali wa soka ya wanawake na wanaume.

Mitandao ya kijamii mbalimbali nchini Marekani, ilikuwa ikijadili hali hiyo, ya kuwa nani mkali katika kusukuma kabumbu japo inabakia tu, wanaume ni zaidi ya wanawake.

Wanaume wanakubalika kwa soka, japokuwa wanawake na wao wanatunisha msuli.

Soka ya wanawake na wanaume

Inaelezwa kuwa soka inayochezwa na wanawake na wanaume ni ileile inayotumia Sheria 17 za Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa.

Pamoja na kwamba wote wanatumia utaratibu unaotakiwa kwa sheria za soka, lakini kwa mwanaume, inabakia kwa mwanaume tu.

Hata mwanamke awe anatisha vipi katika soka, hamfikii mwanaume kutokana na mambo mbalimbali ya asili, mazingira na maumbile kama ilivyokuwa ikielezwa kwenye mitandao mbalimbali.

Jarida moja la utafiti wa soka nchini Marekani, linasema kwa soka wanayocheza wanaume na wanawake, ina tofauti kubwa. Tofauti zinazotajwa:-

Kwanza: Limewasifu wanawake wanaocheza kuwa wanastahili sifa kwa kuthubutu kucheza soka, kwa kuwa sehemu kubwa mchezo huu umezoeleka kwa wanaume pekee.

Mpira uliopotea

Tofauti zinazotajwa ni kwamba; wanaume wanapopoteza mpira, hufanya jitihada za kuusaka mpira ikilinganisha na wanawake. Wanawake wachache wanaweza kufanya hivyo, lakini wengi wao, hata kama adui ana mpira, hawafanya jitihada za kweli kusaka mpira.

Ufundi

Soka ya wanaume ni ya ufundi sana. Wanaume wana uwezo mkubwa wa kimiliki mipira, kiungo hutumia akili sana na humiliki mipira kikamilifu, lakini timu za wanawake, mfano timu ya taifa ya wanawake ya Marekani wakati fulani ilishiriki Kombe la Dunia, kiungo wake alionekana hawezi, hana ufundi na timu nzima haikuwa katika mchezo.

Ujuzi wa kiufundi

Wanaume wanacheza soka ya ufundi mno (hasa mabeki) wana utaalamu zaidi wa kuuchezea mpira kuzuia washambuliaji kuliko wanawake. Inaelezwa kuwa wanaume wana uwezo mkubwa wa kumiliki na kukaa na mpira kwa muda mrefu kuliko wanawake ambao wakati mwingine hupiga bila mwelekeo.

Kasi na haraka

Ni sifa nyingine kwa wanaume, inaelezwa kwamba soka ya wanaume ni ya kasi ikilinganisha na wanawake. Hiyo ina maana mabeki wanakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwa kuwa na wao wanacheza muda wote kuzuia kasi ya washambuliaji. (Wachezaji wanacheza, wanapasiana na ufundi na pasi ni za uhakika).

Hata Ligi Kuu ya England, EPL timu zinacheza kwa spidi kali.

Kukokota Wanawake hushindwa kukokota mipira kwa muda mrefu. Mwanaume ana uwezo kutoka pembe na pembe ya uwanja akikokota ndinga na hata akapiga krosi akiwa kwenye kasi.

Kushindana kwa dhati

Sehemu kubwa ya wanaume katika timu hushindana kwa nguvu na hata kupata ubashiri wa timu gani inacheza fainali, tofauti na wanawake, mwendo wake ni wa kudokoadokoa na wakati mwingine huwezi kujua timu inayoingia robo fainali au nusu fainali au fainali.

Mashabiki

Wachezaji wa timu za wanaume wana mashabiki wengi, wanapata pesa nyingi ikilinganisha na wanawake. Wanaume wanacheza zaidi na kama mchezaji akiwa wa kulipwa, anaongeza nguvu kujifua, na kuwa wa aina yake kuliko mwanamke.

Vitu adimu

Wanaume wanakuwa na vitu vya ziada uwanjani. Wakati mwingine, mechi kubwa huamuliwa kwa idadi ndogo ya magoli. Kwa wanaume pia utaona vichwa vya ‘diving’ tofauti ambavyo huwezi kuona kwa wanawake.

Waamuzi

Uwezo katika uamuzi. Duniani kote, hakuna timu inayosifia waamuzi. Lakini soka ya sasa inaendelea kukua, na zaidi ni waamuzi wanaume ndio wenye uwezo mkubwa katika kuchezesha.

Wanawake hubabaika na kushindwa kutoa uamuzi katika mechi ngumu, iliyojaa ufundi.

Mechi laini

Wataalamu wa soka wanasema pia kuwa mchezo wa wanawake ni laini ikilinganisha na wanaume, ambao una kashkash nyingi.

Majeruhi

Huwezi kukuta majeruhi sana kwa wanawake, lakini njoo kwa wanaume, utakutana na majeruhi wengi.

Hadaa

Wanaume wana uwezo wa kumlaghai refa kwa kuongopa kuumia na kupoteza muda ikilinganisha na wanawake.

Wanawake ni wakarimu hakuna ‘makashkash’ uwanjani kwa sababu mapafu ya wanawake ni madogo kuliko wanaume. Mapafu ya wanawake huingiza kiasi kidogo cha oksijeni ikilinganisha na wanaume.

Kuchoka

Wanasoka wengi wanawake hawana uwezo wa kucheza kwa kasi na licha ya kuwa wanatumia dakika 90, huchoka mapema.

Utafiti unaonyesha kuwa mwanaume hutumia misuli mingi zaidi ya mwili kuliko mwanamke.

Kwa mabeki wa kike, hawana uwezo wa kulinda eneo la penalti na ndiyo maana hupitwa na kufungwa kirahisi ikilinganisha na wanaume.