Kuondoa wakurugenzi ni mwanzo, wasema wadau

Dar es Salaam. Serikali imesema inafikiria kukata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu iliyofuta mamlaka ya wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi, lakini wanaharakati na vyama vya upinzani wamesema bado hatua zaidi zinafuata.

Mahakama ilisema kitendo cha wakurugenzi hao kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Uchaguzi (NEC) ni kinyume cha Katiba inayotaka chombo hicho kuwa huru. Pia imesema Sheria ya Uchaguzi haihakikishi kwamba wakurugenzi hao watakuwa huru katika kutekeleza majukumu yao.

Kesi hiyo ya kikatiba ilifunguliwa mwaka jana na mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe, akipinga wakurugenzi hao wa halmashauri za wilaya, manispaa au majiji kuwa wasimamizi akidai ni kinyume cha Katiba na kwamba ni makada wa chama tawala cha CCM.

Lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi alisema bado Serikali inatafakari hukumu hiyo ili kujua hatua itakayofuata.

“Suala la rufaa ni la kufikiria kwa sababu ni haki. Nafikiri kama Mahakama Kuu haijatoa tafsiri sahihi, basi tutakata rufaa, lakini bado tunazungumza.

“Ndiyo, tatizo la kujaribu hatua inayofuata, yaani hiyo ni hatua ya tano kabla ya hatua ya kwanza hatujaikamilisha. Ngoja tuangalie kwanza halafu tutatoa tamko.”

Ushindi huo wa Wangwe umepokewa vizuri na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (HLRC), ambacho ndicho kilianzisha kesi hiyo.

“Huo ni mwanzo tu,” alisema mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga.

“Bado tunafikiria kufungua kesi nyingine ya kikatiba ya kutaka tume huru zaidi au mchakato wa Katiba urejeshwe ili kuwe na tume huru zaidi.”

Henga alisema huo ni mwendelezo wa mapambano ya demokrasia na haki za kiraia wanazopigania.

“Sisi ndiyo tulikuwa na wazo la kufungua hiyo kesi, tukamtafuta huyo petitioner Wangwe akakubali. Katika kuongeza nguvu tukamwongeza Fatma Karume kwa kuwa yeye ni wakili maarufu,” alisema Henga.

Alisema walikuwa wakipinga kifungu kinachowapa mamlaka wakurugenzi wa wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi, kwa sababu hao ni wateule wa Rais ambaye uchaguzi unaofuata naye anakuwa mgombea. Alisema sababu ya pili ni wakurugenzi hao kuwa makada wa CCM walioshindwa kwenye chaguzi mbalimbali katika chama hicho na hivyo kutokuwa huru wanapokuwa wasimamizi.

“Ma-DED wengi walioteuliwa walikuwa wagombea wa CCM, sasa kwa kuwa kura hazikutosha wakapewa ukurugenzi labda wa Nkasi au wapi, kwa hiyo tukaona hawatatoa haki kwa vyama vingine,” alisema Henga.

Mbali na wanaharakati, makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari ambaye amewahi kuandika kitabu cha Haja ya Kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, alisema hiyo ni hatua muhimu lakini bado kuna haja ya kupambana zaidi.

“Mimi nashukuru kwa sababu nimeanza zamani. Tukiwa CUF nilimshauri Profesa (Ibrahim) Lipumba tususie uchaguzi, akasema hatuwezi kumsusia nguruwe shamba la mihogo,” alisema.

“Nimekwenda Chadema hiyo ndiyo ajenda yangu tangu alipokuwepo Dk (Wilbrod) Slaa. Wenzangu wakaona kama bado, lakini sasa wameona ni muhimu.”

Hata hivyo, alisema hiyo bado ni hatua ndogo.

“Ni kama baharini bado kuna iceberg (theluji). Hilo ni tatizo mojawapo, yapo mengi sana. Ni sawa na kuwa na funza 50 ukimtoa funza mmoja, japo inasaidia, lakini wakurugenzi ndio walikuwa wanabadilisha matokeo kabisa,” alisema.

Alisema Chadema wana kesi nyingine walizofungua, ikiwa ni pamoja na katazo la kutofanya mikutano ya hadhara na maandamano.

Naye kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe alisema huo ni uamuzi wa kihistoria katika ukuaji wa demokrasia nchini.

“Ni wajibu wetu vyama vya siasa kuhakikisha hukumu hii inatekelezwa kwa namna yoyote ile,” alisema.

Akichambua hukumu hiyo, wakili maarufu nchini, Dk Onesmo Kyauke alisema kwa sasa Tanzania inapaswa kuiga mifano ya nchi zenye tume huru za uchaguzi kama Kenya.

“Uteuzi wa viongozi wa tume huru kuanzia mwenyekiti, wajumbe na mtendaji mkuu wakishaorodhesha, majina yanapelekwa hadharani ili wananchi watoe maoni yao,” alisema.

“Baada ya maoni kuzingatiwa, majina yanachujwa na kupelekwa kwa Rais ili wateuliwe.”

Dk Kyauke alishauri kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ili kuiruhusu NEC kuteua wasimamizi ambao pia watatolewa maoni na wananchi kabla ya kupitishwa.