Kura ya maoni yaupa nafasi upinzani Australia

Thursday May 16 2019

Sydney, Australia. Chama cha upinzani cha Labour kinaweza kushinda uchaguzi mkuu wa Australia mwishoni mwa wiki, kura ya maoni imeonyesha jana.

Kwa mujibu wa kura hizo inayofuatiliwa sana, chama cha Conservative cha Waziri Mkuu, Scott Morrison, kinashindwa kuwavutia wapigakura kwa sera yake ya kuimarisha uchumi.

Kura hiyo iliyoendeshwa na gazeti la The Guardian inaonyesha Chama cha Labour kilikuwa mbele ya Cenvervative kwa asilimia 51.5 kwa 48.5 vilipopambanishwa kwa mtindo wa vyama viwili vinavyokubalika, kwa wapigakura kusambazwa hadi mshindi apatikane.

Kura hiyo ni moja ya vipimo vya mwisho vya Waziri Mkuu Morrison kuwa karibu na wapigakura ambao hawakuwa upande wake katika kampeni zake, kuwa Labour itaharibu uchumi ambao kwa miaka 28 umeendelea kukua.

Morrison ameelekeza kampeni yake kwenye matazamio ya Serikali kuwa na bajeti ya kwanza yenye mapato kuzidi matumizi kwa miaka 10 iliyopita.

Chama cha Labour ambacho kilishindwa uchaguzi mara mbili mfululizo mwaka 2013 na 2016, kimeahidi kufikia  mapato yanayozidi matumizi mwaka 2019/20 na kuongeza zaidi mwaka 2020/21.

Kiongozi wa Labour, Bill Shorten amewahakikishia wapigakura waliokata tamaa, vijana na wazee na kuahidi kufanya mfumo wa kodi kuwa wa haki na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Reuters, Morrison na Shorten walitarajiwa jana kutoa hotuba zao za mwisho ili kujaribu kuwashawishi ambao hawajaamua nani wanampigia kura.

Hotuba hizo zinakuja wakati gazeti la Australian Financial Review likiungana na karibu magazeti yote makubwa nchini humo kumuunga mkono Morrison.

 

Advertisement