Kushinda kutwa nzima katika moshi wa mkaa na kuni sawa na kuvuta pakiti mbili za sigara

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makumu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba akiandika maoni yaliokuwa yakitolewa na wadau wa mazingira waliokuwa wakichangia mjadala wa Jukwaa la Fikra linalojadili matumizi ya mkaa, uchumi na mazingira yetu, jijini Dar es Salaam, leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema kutwa nzima mtu akiwa katika moshi unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni ni sawa na kuvuta pakiti mbili za sigara

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema kutwa nzima mtu akiwa katika moshi unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni ni sawa na kuvuta pakiti mbili za sigara.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 7, 2019 katika mdahalo wa Jukwaa la Fikra linaloendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano wa ITV,  Redio One kwenye ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.

Makamba amesema gharama za kiafya kutokana na uharibifu wa hewa unaotokana na mapishi ya kuni na mkaa ni  dola 1.8 milioni ya Marekani kwa mwaka.

Amesema kuwa katika mambo yaliyofanyiwa utafiti, makongamano, semina nyingi ni pamoja na matumizi ya mkaa lakini limechanganya watu kwa sababu lina mbadala mpana.

"Jukwaa hili litatupeleka kwenye uelewa mmoja kuhusu hili jambo na hatua za kuchukua ili sisi kama jamii na Serikali tuweze kuchukua hatua," amesema Makamba.

Amesema kuwa kuna ubishi miongoni mwa wasomi wanaodai kuwa wakulima, wafugaji ndiyo waharibifu wakuu wa misitu mbali ya mkaa.

Amefafanua kuwa kwenye tafiti zote alizosoma hakuna aliyeandika kuwa mkaa unaharibu mazingira chini ya asilimia 50 ni kuanzia hapo hadi asilimia  90.

Amefafanua kuwa mwendelezo ni kuhamasisha mbadala kwa njia ya kisera, kibiashara na kikodi na Serikali ikiangalia masuala ya gesi.

Amesema miaka miwili iliyopita ulifanyika utafiti jijini Dar es Salaam uliohusu aina ya matumizi ya nishati ya kupikia  na kubaini asilimia 88.2 walikuwa wanatumia mkaa jijini Dar es Salaam, 2018 bado ilikuwa matumizi ni asilimia 88.

Ameeleza kuwa miaka mitano nyuma matumizi ya gesi yalikuwa ni asilimia 26 baadaye asilimia 58 hivyo matumizi ya gesi yanaongezeka kwa kasi mno. 

"Miaka mitano iliyopita tulikuwa tunaingiza tani za gesi 28,000, lakini sasa tunaagiza tani 100,000 bei inashuka" amesema.

Amefafanua kuwa sekta binafsi ina nafasi ya kuingilia kati kutengeneza mkaa mbadala ili kuuondoa uliopo kwa kushindana bei sokoni.

"Miaka mitano nyuma hakukuwa na mkaa mbadala , lakini sasa zipo kampuni zimenunua mashine na kutengeneza mkaa na unatumika, mkaa hatutaupiga nyundo, utaondoka sokoni kutokana na upinzani wa bei,” amesema Makamba.