UCHOKOZI WA EDO: Kutana na jamhuri ya muungano ya bodaboda

Monday April 15 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

Umewahi kuisikia jamhuri ya muungano ya watu wa bodaboda? Ipo hapa nchini. Huwa inapimana ubavu na utawala wa Namba Moja. Huwa nacheka sana. Namba Moja anatawala nchi kivyake na wao wanataka kutawala kivyao.

Waendesha bodaboda wamekuwa na nguvu kubwa. Wana maamuzi makubwa katika matukio yanayowahusu. Wao ndio polisi, wao ndio waendesha mashtaka, wao ndio mahakimu. Usiombee kukumbana na makali yao.

Umewahi kuona mwenzao akipata ajali? Huwa hawajali sana nani amesababisha. Wanamkimbiza na kumpiga aliyehusika katika ajali ya mwenzao. Huwa hawana muda wa kujadili nani amesababisha ajali. Huwa hawana muda wa kumsubiri trafiki afike eneo la tukio.

Watu wengi hunusuru roho zao kwa kukimbia pindi wanapohusika katika ajali na bodaboda. Wanajua kwamba ghafla hutokea ushirikiano wa ajabu miongoni mwao, hata kama hawajuani, na wanatoa hukumu hapo hapo kwamba mwenzao ameonewa.

Ukiwa unabishana na dereva mmoja wa bobaboda kwa sababu yoyote ile, wenzake huwa hawawezi kupita hivi hivi. Hata kama hawamjui watajitokeza na kuanza kumtetea. Ukizubaa wanaanza kukupiga bila ya kuelewa sababu ya ugomvi wenu.

Watu wa bodaboda wanatamba sana. Umewahi kuwaona wakiwa wanaenda katika mazishi ya mwenzao? Unaweza kudhani ni msafara wa Namba Moja. Huwa wanaichukua barabara yote. Bodaboda zinaweza kuwa kama 100 hivi. Wanapiga honi huku wanaendesha kwa kasi. Hawajali chochote kile.

Sijui ni namna gani tunaweza kushughulika na huu muungano wao lakini tayari wamejijenga kwa kiasi kikubwa. Ushirikiano wao ni kama ule wa wavuta sigara. Hawahitaji kujuana ili wasaidiane. Ili mradi wote wapo katika fani moja basi kila mmoja yupo tayari kufa kwa ajili ya mwenzake.

Mamlaka husika inabidi zianze kuitupia macho hii jamhuri yao ya muungano. Sijui zitafanyaje kuwadhibiti pindi mambo yanapomuendea kombo raia lakini hawa jamaa wanazidi kuwa hatari siku hadi siku.

Ukiingia katika anga zao unaweza kujuta kwa muda wote wa maisha yako hata kama wamekuachia roho yako salama. Ushirikiano wao ni kitu cha kushangaza pia.

Advertisement