Kutekwa kwa raia wa Kenya, Zitto aiomba Serikali ya Tanzania

Muktasari:

Leo Jumatatu, Raphael Ongagi ambaye ni raia wa Kenya ametimiza siku ya saba tangu alipotekwa na watu wasiojulikana maeneo ya Oysterbay, Dar es Salaam, Tanzania Juni 24, 2019. Kiongozi wa chama cha upinzani n chini Tanzania cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka waliomteka kumwachia akiwa hai.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe ameitaka Serikali ya Tanzania kuangalia kwa uzito suala la kutekwa kwa raia wa Kenya anayeishi Tanzania, Raphael Ongagi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Julai 1, 2019 jijini Dar es Salaam, Zitto amesema masuala ya utekaji yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa nchi ya Tanzania.

Amesema Tanzania haipaswi kuwa na taswira hiyo kwa mataifa mengine hasa nchi jirani ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo katika mambo mengi.

Akizungumzia mazingira ya kutekwa kwake, Zitto amesema siku aliyotekwa maeneo ya Oysterbay, Dar es Salaam Juni 24, 2019 Raphael alikuwa na mke wake Veronica wakitokea shuleni kwa mtoto wao kwenye kikao cha wazazi.

“Gari moja iliwazuia kwa mbele na kuwatolea silaha aina ya bastola na kuwachukua wote wawili kabla ya kumwachia mkewe na kuondoka na Raphael. Leo (Jumatatu) ni siku ya saba hatujamwona Raphael,” amesema Zitto

Kiongozi huyo wa chama hicho ameweka wazi kwamba hakuna taarifa zozote zinazomhusu (Zitto) ambazo Raphael anazifahamu kwa kuwa kuna habari kuwa watekaji wanataka kupata taarifa zake.

“Napenda kuwaambia watekaji kwamba hawawezi kupata taarifa zozote kunihusu mimi (Zitto) kupitia kwa Raphael. Hana taarifa zozote ambazo anaweza kuwapa kwa hiyo watamuumiza bure naomba wamuachie,” amesema Zitto

“Kama kuna taarifa zozote ambazo wanadhani zina makosa au jinai waniite mimi mwenyewe nikawape taarifa hizo, wamuache akaendelee na maisha yake ya na familia yake.”

Akimzungumzia Raphael, mbunge huyo amesema kijana huyo alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akiwa nchini Tanzania amekuwa na marafiki wengi Watanzania na hata amefunga ndoa na Mtanzania, Veronica Kundya.

Zitto amesema Raphael ana watoto wadogo wawili ambao wiki moja sasa hawajui baba yao yupo wapi.

Amesema tangu mwaka 2009 mpaka mwaka 2016 Raphael alikuwa akifanya kazi naye (Zitto) akiwa msaidizi wangu. Hata baada ya kuamua kufanya biashara za usafirishaji, Raphael aliendelea kuwa mtu wa karibu yangu mpaka alipotekwa Juni 24 mwaka 2019.