Kwa nini Dunia inawahitaji kina Liquid

Dar es Salaam. Wakati magaidi waliposhambulia ubalozi wa Marekani nchini, kuna watu walifurahi kwamba angalau Tanzania itapata umaarufu japo kwa tukio baya baada ya vituo karibu vyote vya televisheni duniani kutangaza taarifa za tukio hilo.

Ndivyo sehemu au binadamu anavyopata umaarufu; kwa mazuri, mabaya, vituko au jambo jingine lolote linalosisimua au kuvuta hisia. Huo ndio huwa mwanzo wa safari ya mafanikio kwa kuchukua mkondo tofauti.

Na dunia ya leo, ambayo teknolojia ya mawasiliano inakua kwa kasi; dunia ambayo uhuru wa kujieleza unaminywa na hali ya uchumi kuwa ngumu, faraja pekee katika jamii yaweza kuwa ni watu wanaosisimua, kufurahisha, kugusa hisia au kuzungumzia mambo magumu katika lugha nyepesi.

Miongoni mwa watu hao ni Liquid, ambaye si msanii, si mwanamuziki, si mwanamichezo na wala si muigizaji, bali mwenye mambo ambayo yanazungumza lugha ya Watanzania wa sasa.

Liquid hatofautiana na Mwisho Mwampamba, Richard Dyle Bezuidenhout au Iddris ambao walipata umaarufu barani Afrika kwa kuwa kituko katika kipindi cha Big Brother. Baadhi wamechukua mkondo tofauti wa maisha baada ya kujengewa msingi na umaarufu huo.

Na Liquid ndio kwanza ameanza safari ya umaarufu, ambao umemfanya atamkwe na watu maarufu kama Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Spika Job Ndugai.

Dunia imeamua hivyo

Kutoka kwa mwanamitindo na mtangazaji maarufu wa vipindi vya televisheni vya mazungumzo, Kim Kardashian wa Marekani mpaka Wema Sepetu wa Tanzani, taswira inayoonekana ni moja tu; dunia kukumbatia watu wanaoleta kitu tofauti katika jamii.

Na umaarufu wao unavuka mipaka kutokana na uwezo wa teknolojia ya mawasiliano iliyogeuza dunia kuwa kijiji.

Awali, watu walidhaniwa kuwa hawana thamani mbele ya jamii kutokana na kutumia muda mwingi katika mambo yanayoonekana kuwa ya hovyo, kuzungumzia mada zisizoangalia masuala magumu kama ya uchumi, maendeleo, sheria na mengineyo, lakini sasa wamekuwa kipenzi cha dunia.

Na katika baadhi ya nchi kama Ukraine, wananchi wanataka mtu wa aina hiyo ndio apewe nchi, yaani mchekeshaji Volodymyr Zelenskiy anayesubiri hatua ya pili kabla ya kutangazwa kuwa rais baada ya kushinda duru la kwanza kwa kura nyingi, akimuacha mbali rais wa sasa.

Hivi sasa mtu anayeitwa Liquid, aliyejizolea umaarufu katika mitandao ya kijamii ambako video zinamuonyesha akiwa baa anakunywa, ndiye gumzo karibu kila kona ya nchi na kila mtu anataka kuwa karibu naye.

Na jana alikuwa bungeni kushuhudia shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria, akiwa amekaa sehemu ya wageni wa hadhi ya V.I.P.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anaweza kuwa ndiye aliyezidisha umaarufu wa watu wa aina hiyo, aliposhauri waandishi wa habari kuacha kuzipa uzito habari za watu ‘wasio na maana’ kama Konki Liquid Pierre, ambaye jina lake halisi ni Peter Molel.

Makonda alisema hayo Jumamosi katika halfa iliyoandaliwa na mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, yenye lengo la kuhakikisha wahitimu wote wa kidato cha nne wanafaulu, ikipewa jina la “Tokomeza Zero Kisarawe”.

“Yaani unakuwa na taifa ambalo watu wa hovyo ndiyo wanakuwa maarufu halafu watu wa maana hawajulikani walipo,” alisema Makonda.

“Huwezi kuwa na taifa lina-promote watu wa hovyo mpaka wanakuwa mabalozi. Unategemea watoto wetu watafika kwenye mafanikio kweli? Nadhani watu kama hawa wanapaswa kupewa sapoti siyo hao walevi mnaotutangazia.”

Hapo ndipo ilipodhihirika kuwa dunia inamtaka zaidi Liquid baada ya kuibuka mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii. Wengi walijitokeza kumtetea Liquid na kumkosoa RC huyo kwa kauli yake dhidi ya watu wa aina ya Liquid, ambaye ni mkazi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Maoni ya watu hao ni ujumbe tosha kwa Makonda na wengine wenye mtazamo kama huo, kuwa dunia ya sasa imeshikwa na watu wa aina ya akina Kim Kardashian, Liquid, Zelenskiy, Dk Shika au Jimmy Morale, mchekeshaji aliyeshinda uchaguzi wa rais wa Guatemala.

Viongozi wenye nguvu katika uamuzi mkubwa wa dunia, si maarufu katika mitandao ya kijamii, kuanzia Vladimir Putin wa Russia, Angela Merkel (Ujerumani), Theresa May (Uingereza) mpaka Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Lakini, watu wenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii ni wanamichezo, wasanii, wanamuziki, wachekeshaji na wacheza filamu ambao wengi wao hawakwenda shule au elimu yao ni ndogo, na wanaoonekana katika video za vituko kama ilivyokuwa kwa Dk Shika na sasa Liquid.

Hao ndio wanafuatiliwa na watu wengi katika mitandao ya kijamii kama Twitter, Instagram na Facebook.

Yaani, hata vyombo vya habari vikiwapuuza, bado mambo yao yatafuatiliwa na wafuasi hao lukuki ambao huongezeka kila kunapotokea kituko.

Ndio maana haikuwa ajabu kwa uongozi wa Bunge kumualika Liquid kushuhudia shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria, siku moja baada ya kusema chombo hicho hakiko tayari kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), ambaye taarifa zake huliwezesha Bunge kuisimamia Serikali kikamilifu.

Na kwa kulijua hilo kampeni mbalimbali za kisiasa katika nchi mbalimbali duniani, watu hao wamekuwa wakishirikishwa kwa lengo la kuongeza mashabiki na wapiga kura.

Ingekuwa ngumu watu hawa kukubalika miaka 20 iliyopita, pengine walionekana watu wa hovyo na wasio na elimu, lakini kadiri teknolojia ilivyoipeleka dunia kasi, watu hawa wamekuwa muhimu sana katika kuibadili dunia na watu wake.

Mwanamuziki wa Marekani, Beyonce alitumia nguvu kumpigia debe seneta wa Democratic, Beto O’Rourke kama Rihanna alivyofanya kampeni katika Jimbo la Florida kwa Andrew Gillum wa Democratic.

Maisha yanavyokwenda kasi na teknolojia ikiwa juu, watu hawa wamekuwa chachu ya mabadiliko hayo na ndio maana hata taasisi kubwa za kimataifa zimekuwa zikiwatumia kama mabalozi wao katika shughuli mbalimbali.

Pengine kutokana na watu kuchoshwa na siasa zinazoonekana kama za ‘maigizo’, huenda wameamua kuwasikiliza zaidi waburudishaji kuliko wanasiasa.

Sehemu pekee ambayo mtu hawezi kusumbuliwa kujadili ni sanaa, michezo, filamu na burudani.

Hiyo inaweza kuwa sababu ya watu kuhamishia mtazamo katika mambo hayo kiasi kwamba watu wanaoshiriki katika matukio hayo wamekuwa maarufu zaidi na wenye ushawishi.

Katika uchaguzi uliopita nchini, wasanii walitumika katika kampeni za vyama mbalimbali, lakini chama tawala ndicho kililamba dume na hata kuwa na wasanii karibu wote, kama Steve Nyerere na Diamond Platinumuz.

Watu hao hawajaishia kuwa chachu ya mabadiliko tu, wamekuwa wanagombea nafasi mbalimbali na kushinda uchaguzi mfano mzuri ni Sugu, ambaye mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Haule (Mikumi).

Hata majuu, mcheza filamu maarufu duniani, Arnold Schwarzenegger alikuwa gavana wa Republican wa Jimbo la California kwa vipindi viwili kuanzia mwaka 2003 na vyombo vya habari vilipenda kumuita ‘Governator’ kutokana na filamu zake za Terminator.

Katika nchi jirani, Robert Kyagulanyi Ssentamu ‘Bobi Wine’ ni mwanamuziki wa Uganda wa mtindo wa dancehall ambaye sasa ni mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki.

Pengine jamii imeamua kuachana na siasa ngumu kwa sababu wanaona hawawaelewi wanasiasa na hivyo hawapati kile “kitu roho inapenda”, ambacho Liquid na wenzake wanaweza kuwapa hata wakikurupushwa usingizini.