LHRC yajitosa sakata la Mdee, yatoa neno kwa IGP na msajili wa vyama

Muktasari:

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania kimelitaka jeshi la polisi kumwachia huru mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee au kumfikisha Mahakamani mara moja kujibu tuhuma zinazomkabili.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Tanzania kimetoa wito kwa jeshi la polisi kumwachia huru mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee au kumfikisha Mahakamani mara moja.

Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), anashikiliwa tangu jana Jumapili Julai 15, 2019 katika kituo cha polisi Bukoba mkoani Kagera ambako alikuwa na mkutano wa ndani na wanawake wa Chadema katika mkoa huo.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatatu Julai 15,2019 Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema tukio la kuzuiliwa kwa mikutano ya wapinzani ni mwendelezo wa ukandamizaji wa haki za kisiasa hapa nchini kwa mwaka wa tatu sasa.

"Tunalitaka jeshi la polisi kumpatia dhamana Mdee na kumfikisha mahakamani badala ya kumshikilia bila kufuata taratibu za kisheria za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa," amesema Henga.

Mkurugenzi huyo amemsihi Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kusimamia na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, sera, kanuni na weledi.

Pia, ametoa wito kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuwajibika kama mlezi wa vyama vya siasa na kusimamia usawa wa vyama katika kutekeleza shughuli zao bila ubaguzi.

Jana Jumapili, Mdee  mara baada ya kumaliza mkutano wa ndani wa wanawake mjini Bukoba mkoani Kagera alichukuliwa na polisi hadi kituo kikuu cha mkoa huo ambako baadhi ya viongozi waliokuwa naye walihojiwa na kuachiwa huku yeye (Mdee) akiendelea kushikiliwa.