LHRC yalia na polisi uchunguzi shambulio la Lissu, uvunjifu haki za binadamu

Muktasari:

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema Jeshi la Polisi nchini Tanzania  linasababisha maswali mengi kuliko majibu katika uchunguzi wa matukio mbalimbali ya mauaji na watu kutekwa


Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema Jeshi la Polisi nchini Tanzania  linasababisha maswali mengi kuliko majibu katika uchunguzi wa matukio mbalimbali ya mauaji na watu kutekwa.

Amesema ni kutokana na baadhi ya matukio uchunguzi wake kutowekwa wazi, ikiwa ni pamoja na wahusika kukamatwa, huku akitolea mfano tukio la shambulio la Tundu Lissu.

Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge. Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, 2018 alipohamishiwa Ubelgiji alikotibiwa hadi Desemba 31, 2018. Kwa sasa yupo katika ziara Ulaya na Marekani huku akieleza kuwa licha ya kuruhusiwa bado anaendelea na matibabu na hivi karibuni atafanyiwa operesheni nyingine.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kuwashangaa polisi kutomkamata Lissu hadi sasa, huku akibainisha kuwa mbunge huyo na dereva wake ndio mashahidi muhimu.

Alipoulizwa kauli hiyo ya mkurugenzi wa LHRC, msemaji wa Jeshi la Polisi Ahmed Msangi amesema hawezi kujibu maswali hayo huku akimtaka mwandishi ampe muda ili apate takwimu za matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na jinsi yanavyoshughulikiwa na polisi.

Katika maelezo yake Henga amesema matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binadamu yamekuwa makubwa kutokana na kasi ndogo ya utendaji wa Polisi.

“Kwa mfano mauaji yaliyotokea mkoani Njombe na Simiyu. Polisi hawachukui hatua mpaka jamii ilalamike sana, kama hailalamiki hatua haziuchukuliwi. Kitu ambacho siyo sahihi, kwa sababu Katiba inatamka Serikali ndiyo mlinzi wa wananchi,” alisema Henga.

Amesema wamekuwa wakitoa matamko pale ambapo Jeshi la Polisi limeshindwa kuchukua hatua ikiwa pamoja na kuwanadikia taarifa za matukio hayo.

“Kwa sasa timu zetu ziko mikoa ya Njombe na Simiyu zinakusanya taarifa ili tuendane na wakati. Lakini tumekuwa tukitoa matamko na kuandika taarifa polisi kuhusu matukio hayo,” alisema Henga.