Latra: Ufuatiliaji mwendo wa mabasi haujasitishwa

Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imesema utaratibu wa kufuatilia mwendo wa mabasi nchini Tanzania haujasitishwa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imesema utaratibu wa kufuatilia mwendo wa mabasi nchini Tanzania haujasitishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Julai 18, 2019 baada ya kumalizika kwa kikao cha Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), mkurugenzi wa udhibiti wa barabara, Johansen Kahatano amesema katika kipindi cha wiki mbili yameripotiwa matukio ya mabasi kutembea mwendo wa kazi.

"Katika kukabiliana na changamoto hiyo mamlaka imeitisha kikao cha dharura na kamati tendaji ya Taboa na kuazimia mambo mbalimbali," amesema Kahatano.

Amesema mfumo wa kuratibu mwendo wa mabasi upo na unaendelea kutumika kuyafuatilia na wahusika kuchukuliwa hatua.

Amesema Latra inatoa angalizo kwa wamiliki wa mabasi yanayowahi kuondoka  kabla ya muda na kusababisha ushindani usio na usawa.

"Ili kutafuta suluhu ya kudumu ya kudhibiti mwendo, Latra itakutana na kampuni zinazowakilisha watengenezaji mabasi kuangalia uwezekano wa kusanifiwa na kuwekewa ukomo wa mwendokasi kutoka kiwandani," amesema.

Katibu mkuu wa Taboa,  Enea Mrutu amesema taarifa za mwendokasi huo zimewasikitisha na kuahidi kukemea  matukio yote ya ukiukwaji wa sheria barabarani.