Lema: Tumemuondoa Zitto usiku, alikuwa akifuatiliwa

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akichangia mjadala wa Taarifa mbili za Kamati za kudumu za Bunge zilizowasilishwa bungeni jijini Dodoma leo ikiwa ni Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema juzi Jumatano Februari 6, 2019 walilazimika kumuondoa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe sehemu waliyokuwa baada ya kufuatiliwa na watu ambao hakuwataja

Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema juzi Jumatano Februari 6, 2019 walilazimika kumuondoa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe baada ya kufuatiliwa na watu ambao hakuwataja.

Akizungumza wakati akichangia taarifa ya kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria leo Ijumaa Februari 8, 2019,  Lema amesema  kama CCM wakitawala kwa haki, kwa kufuata sheria na Katiba hana tatizo hata wakitawala milele.

“Lengo letu ni kuwaona mnatutawala kwa haki na ndio maana ya upinzani lakini leo hii chuki inajengwa leo kiongozi mmoja M-NEC anasema Lissu (mbunge wa Singida Mashariki) akitua ashambuliwe,” amesema Lema.

“Leo mwenyekiti (Mussa Azzan Zungu),  Zitto  hayuko bungeni tumemuondoa juzi alikuwa anafuatiwa usiku kwa kazi za kibunge sio za kuuza madawa ya kulevya si

za kubaka watoto ni kazi za kibunge.”

Akizungumza na Mwananchi alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Lema,  Zitto amesema, “Tukio ni la kweli lakini mimi siwaogopi wafanye watakalo.  Wabunge wenzangu Silinde (David-Momba) na Upendo Peneza (Viti Maalum Chadema)  waliowatambua watu hao  waliniondoa pamoja na Antony Komu (Moshi Vijijini) na  kupelekwa mahala salama.”

Huku akizungumzia matukio yaliyowahi kumkuta ikiwa ni pamoja na kutaka kutekwa Lema amesema, “Leo hii kuna watu wanaozea mahabusu kwa kesi za utakatishaji fedha. Kenya kila kesi ina dhamana kasoro uhaini, Uganda hata uhaini una dhamana ni haki. Dhamana ni haki kuu katika katiba.”

Amewataka  mawaziri na makatibu wakuu kujiandaa kwenda jela ama kubadilisha sheria ambazo zina upungufu.

“Mtafanya mtakachoweza kufanya, tunaweza tusirudi bungeni tena, mkasema tutamuweka mtu wetu atalinda utawala uliopita. Utawala uliopita haulindwi,” amesema Lema.