Lema asimamishwa bungeni hadi mwakani, Spika Ndugai awageukia waliosusa

Thursday April 4 2019

Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza bungeni

Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza bungeni kuhusu adhabu aliyopewa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ya kutohudhuria mikutano mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kulidharirisha Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge kuanzia leo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutamka kuwa Bunge ni dhaifu.

Kabla ya uamuzi huo kupitishwa, wabunge wa Chadema na baadhi ya wabunge wa CUF wakiongozwa na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni,  Freeman Mbowe walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kupinga hatua hiyo, huku Spika Job Ndugai akiagiza kwa siku ya leo wasishiriki kikao cha Bunge kwa kuwa walichagua kutoka nje.

Uamuzi huo umepitishwa leo baada ya mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka kutoa mapendekezo ya kamati hiyo, kuwa Lema asimamishwe kushiriki mikutano mitatu ya Bunge.

“Mnaoafiki mapendekezo ya kamati mseme ndio, msioafiki mseme sio,” amesema Ndugai na kuongeza “Wote mmeafiki Lema anafungiwa kutohudhuria mikutano mitatu ijayo ya Bunge.”

“Hatuwezi kumkunja samaki mkavu lazima twende naye jinsi alivyo. Anafungiwa mikutano mitatu kuanzia huu (wa Bajeti) na mingine miwili itakayofuata.”

 “Huko alipo Lema akiropoka atarudishwa tena katika maadili (kamati ya Bunge). Huyu mtu ana uhakika kuwa hachaguliki kabisa, kama anajua hali ndiyo hiyo na yale niliyosema jana (kukopa fedha) utaacha kupata matatizo kidogo?, lazima utachanganyikiwa kidogo. Demokrasia ni kusikilizana wabunge,” alisema Ndugai.

Advertisement

Kutokana na wabunge hao kutoka nje, Ndugai amesema kwa siku ya leo wasishiriki kikao cha Bunge na kuwaagiza askari wa Bunge kuhakikisha hawarejei ndani.

Juzi Aprili 2 bungeni jijini Dodoma, Lema wakati akizungumzia mapendekezo ya kamati iliyompa adhabu mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema Bunge ni dhaifu.

Mdee alitoa kauli hiyo akiunga mkono iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuwa chombo hicho cha Dola ni dhaifu. Lema wakati akichangia adhabu aliyopewa Mdee juzi bungeni aliunga mkono kuwa Bunge ni dhaifu.

Kutokana na kauli yake hiyo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliagiza kamati hiyo kumhoji Lema na jana Spika Job Ndugai akaagiza kamati hiyo kumhoji saa 8 mchana na kuwasilisha taarifa yake leo ili jambo hilo limalizike.

Baada ya kamati hiyo kutoa mapendekezo hayo, wabunge walipewa nafasi ya kuchangia akiwamo mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika aliyesema kuwa  iwapo adhabu hiyo ya Lema itapitishwa, Bunge halitamtendea haki.

Baada ya Mnyika kumaliza kuzungumza, wabunge wa Chadema na baadhi ya wabunge wa CUF walinyanyuka katika viti na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

“Vipi mbona mnatoa tena,” amesema Ndugai wakati wabunge hao wakitoka nje wakiongozwa na Mbowe.

Awali, akisoma taarifa ya kamati hiyo kuhusu mahojiano na Lema, Mwakasaka alisema Bunge linaongozwa kwa mujibu wa katiba na sheria.

Alisema Lema alipokuwa akichangia hoja kuhusu shauri linalomhusu Mdee naye alisema Bunge ni dhaifu.

“Kwa kuwa kiti kilimpeleka Lema mbele ya kamati ya Bunge kwa ajili ya uchunguzi wa kauli yake ya kulidhalilisha Bunge kuwa ni dhaifu na kwa kuwa kamati ilibaini kuwa Lema amekiuka kifungu cha  26 E cha sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, imemtia hatiani.”

“Hii ni mara ya pili (Lema) anaitwa katika kamati ya maadili. Hata alipoitwa (jana) hakujutia kosa lake na aliendelea kusisitiza kuwa Bunge hili ni dhaifu. Kwa kuwa Lema ni mbunge mkongwe ana ana uelewa wa namna Bunge linavyoendeshwa, kitendo alichofanya ni ukosefu wa heshima,” alisema Mwakasaka.

Amesema kamati hiyo pia ilikataa ombi la Lema la kutaka apewe muda awasiliane na wakili wake kwa kuwa ni mbunge mzoefu na anayejua utaratibu.

“Kutokana na Lema kukiri kuunga mkono kauli ya CAG na Mdee kamati iliona  naye ametenda kosa lilelile. Kamati ilipitia video wakati Lema akizungumza na ikabaini kuwa alitamka kwa makusudi maneno hayo,” alisema.

Advertisement