Lema ataja kitakachopunguza watalii nchini

Mbunge wa Arusha Mjini(Chadema) Godbless Lema akichangia mjadala bungeni jijini Dodoma wa Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Shughuli zilizotekelezwa kwa kipindi cha kuanzia Machi, 2018 hadi Januari 2019

Muktasari:

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema leo Jumatatu bungeni ametaja kitakachosababisha watalii wanaotembelea Tanzania kupungua na kuitaka Serikali kuchukua hatua

Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema amesema kufungwa kwa maduka ya kubadilishia fedha kutapunguza idadi ya watalii kutokana na usumbufu wanaoupata kutokana na hatua hiyo.

Lema amesema hayo leo Jumatatu Bungeni Februari 4, 2019 wakati akichangia taarifa za kamati za Bunge za Miundombinu na Viwanda, Biashara na Mazingira.

Amesema biashara haihitaji nguvu wala polisi ili kuifanikisha na kutoa mfano wa maduka ya kubadilisha fedha yaliyofungwa jijini Arusha miezi miwili iliyopita.

Amesema hakuna duka la fedha linabadilisha fedha jijini humo hivi sasa, ni lazima watalii waende Moshi ama waingie benki kubadilisha fedha.

Hata hivyo, amesema kutokana na usumbufu huo, kampuni za utalii zinaamua kuwahamishia nchi jirani ya Kenya watalii ili kuepuka usumbufu.

Amesema idadi ya watalii itapungua sana mwaka huu na kuhoji inachukuaje miezi miwili kurudishwa.

Amesema kuwa wakidai fedha zao ambazo zimezuiliwa wanaambiwa kuwa watapewa kesi ya kutakatisha fedha.

“Mimi eti wanasema kuwa nina maduka 10 ya kubadilisha fedha. Namuomba Mungu anipe. Usalama unawaingiza chaka,” amesema Lema.