Lema atoa ujumbe baada ya kusimamishwa kuhudhuria bungeni

Gobdless Lema

Muktasari:

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Gobdless Lema leo amesimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge. Sasa atakosa mkutano 15 wa Bajeti unaoendelea, wa 16 utakaofanyika Septemba na wa 17  Novemba 2019

Dar es Salaam. Baada ya Bunge kupitisha azimio la kusimamishwa, Gobdless Lema kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge kuanzia leo 2019, mbunge huyo wa Arusha Mjini (Chadema) amewatakia wabunge wenzake kazi njema.

Katika ujumbe ambao ameuandika katika akaunti yake ya Twittwer, Lema amesena, “Nimesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge mpaka Januari 2020. Moyo wangu una amani sana, kwani mahusiano yangu na HAKI yanaendelea kuimarika zaidi.”

“Nawatakia Wabunge wenzangu kazi njema katika wajibu huu, sitanyamaza hata kama adhabu itakuwa ni mauti.”

Katika ujumbe mwingine Lema amesema, “Msiogope. Mungu aliyetupa macho sio kipofu kwamba haoni, Mungu aliyetupa masikio sio kiziwi kwamba hasikii.”

“Yeye ni Mungu asiyekuwa na msongo wa mawazo kama sisi. Siku imekaribia sana kwa kila mtu kulipa kwa kadri alivyopanda.”

Ujumbe huo  ameutoa baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kupitia mwenyekiti wake, Emmanuel Mwakasaka kuwasilisha taarifa yake baada ya kumhoji mbunge huyo jana kuhusu kauli aliyoitoa kuwa Bunge ni dhaifu ni ya kudhalilisha chombo hicho cha kutunga sheria.