Lilikuwa Bunge la kodi, tozo

Monday February 11 2019

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba  ya

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba  ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma, juzi. Picha na Anthony Siame 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mkakati wa Serikali kutaka kujitosheleza kwa mapato ya ndani umeshuhudia changamoto ya ongezeko la wingi wa kodi na tozo ambazo zilibeba sehemu kubwa ya mjadala kwenye Bunge lililokamilika wiki iliyopita.

Mkutano huo wa 14 wa Bunge la 11 uliohitimishwa juzi jijini Dodoma, ulipokea malalamiko kutoka sekta ya utalii na maliasili, miundombinu, usafiri wa nchikavu na mamlaka ya hali ya hewa pamoja na miradi inayotekelezwa na mashirika ya umma.

Aidha, mkutano huo wa siku 10 ulioanza Januari 29 ulijadili miswada mbalimbali iliyowasilishwa na taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati za Bunge mwaka jana.

Katika taarifa hizo za kamati, tozo na kodi nyingi zinazotozwa na Serikali zilikuwa ajenda kubwa zaidi kiasi cha kutaka kumlazimu Spika Job Ndugai kuitaka Serikali kuzipunguza.

Kabla ya kutangaza kuahirisha mkutano huo hadi Aprili 2 watakapokutana kwenye Bunge la Bajeti ya mwaka 2019/20, Spika aliitaka Serikali baada ya kurekebisha sheria za majengo, madini na zabibu basi iangalie na maeneo mengine.

“Kwa kuwa Bunge lijalo ni la bajeti, marekebisho yaendelee kwa sababu yapo maeneo kadhaa yanahitaji kuangaliwa vizuri ili kuwapunguzia watu mzigo na kuiongezea Serikali mapato. Kuna mahali unapunguza kiwango cha kodi lakini mwisho wa siku unahamasisha kulipwa zaidi,” alisema Ndugai.

Advertisement

Malalamiko ya kodi na tozo yalikuwamo kwenye taarifa zilizowasilishwa na kamati mbalimbali za Bunge zilizobainisha mrundikano unaosababisha baadhi ya biashara kufungwa na nyingine kudumaa kutokana na mazingira ya kibiashara kutokuwa rafiki.

Kamati ya ardhi, maliasili na utalii ilishauri Serikali kuangalia upya utitiri na ukubwa wa tozo kwenye huduma za utalii nchini ili kuiongezea tija sekta hiyo.

Mjumbe wa kamati hiyo, Dk Stephen Kiruswa alisema huduma mbalimbali kwenye sekta ya utalii ni kigezo muhimu katika kuhakikisha inakua na kuongeza fedha za kigeni.

“Kumekuwa na mabadiliko ya tozo jambo ambalo linayumbisha sekta ya utalii nchini,” alisema Dk Kirusa, mbunge wa Longido (CCM).

Mwaka 2016, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ilipewa jukumu la kuhakikisha inawavutia walau watalii milioni tatu ifikapo 2018 kutoka zaidi ya milioni 1.1 walioingia mwaka 2015 lakini haijafanikiwa.

Tanzania ilipokea wageni milioni 1.3 mwaka 2017 licha ya kuwa ya pili kwa wingi wa vivutio duniani ikiwa nyuma ya Brazil. Ubovu wa miundombinu ya usafiri, bajeti ndogo ya matangazo na tozo ya vinyago vinavyonunuliwa na watalii ni changamoto nyingine zinazoikabili sekta hiyo.

Licha ya utalii na maliasili, kamati ya miundombinu ilishauri kufanyika kwa mapitio ya viwango vya tozo katika Daraja la Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam kuruhusu magari madogo ya abiria kumudu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso alisema magari hayo yanalazimika kushusha abiria upande mmoja kukwepa tozo hivyo kusababisha abiria kutembea kwenda upande wa pili kupanda gari jingine.

Daraja hilo lilijengwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambalo lina mkataba wa kulisimamia kurudisha gharama za uwekezaji.

Ilipokuwa inajadiliwa miswada ya Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa na ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu mwaka 2018 hoja ya ukubwa wa adhabu kwa baadhi ya makosa iliibuliwa.

Wabunge walisema faini isiyopungua Sh50 milioni au kifungo cha zaidi ya miaka mitano au vyote viwili kwa mtu anayetangaza utabiri wa hali hewa ni kubwa.

Katika Sheria ya Usafiri Nchi Kavu, faini ya Sh3 milioni kwa mtu mmoja au Sh5 milioni kwa kampuni au kifungo cha miaka miwili jela pia ilielezwa kuwa ni kubwa.

Alipokuwa akiridhia azma ya ubadilishaji hadhi mapori ya akiba ya Biharamuro, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa hifadhi za Taifa, Spika alitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuangalia wingi wa kodi zilizopo kwenye Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) katika miradi inayotekeleza.

“Kodi kila kona na ndiyo maana wanashindwa kuingiza vifaa vipya kwa kuhofia kodi. Sasa mwisho wa siku hata miradi wanayoianzisha inakufa,” alisema Ndugai.

Advertisement