Lipumba: Tutachukua urais Zanzibar mwakani

Sunday April 14 2019

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akisalimiana na wanachama wa Chama hicho Kisiwani Unguja Zanziabar jana kabla ya kuhutubia .Picha na Muhammed Khamis 

By Muhammed Khamis,Mwananchi [email protected]

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ametua Zanzibar na kusema chama hicho kitawashangaza wengi pale kitakapoibuka na ushindi uchaguzi mkuu ujao mwakani kwa nafasi ya urais visiwani humo.

Aliyasema hayo jana kisiwani Unguja wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho katika mkutano wake kwa kwanza tangu kumalizika kesi zilizokuwa mahamakani zikihusisha pande mbili ndani ya chama hicho zilizokuwa zikisigana.

Upande mmoja ulikuwa ukiongozwa na Profesa Lipumba na mwingine na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamadi ambaye ameihama CUF na kujiunga na ACT-Wazalendo pamoja na kundi kubwa la wanachama.

Profesa Lipumba alisema kwa sababu ya ari walionayo viongozi wapya na nguvu kuwa ya wanachama watiifu waliyonayo, ana amini watatimiza ndoto ya wananchi wa Zanzibar kuing’oa CCM madarakani na kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa.

Alisema sababu nyingine itakayopelekea kushinda uchaguzi huo ni mwenendo usioridhisha wa uchumi ndani ya nchi.

“Kwa hali ilivyo sasa ni wazi tukiwafikia wananchi na kunadi sera zetu kwa ustadi mkubwa tutachaguliwa kwa nafasi ya urais na kupata idadi kubwa ya wabunge na wawakilishi maeneo mengi Tanzania,” alisema.

Aidha, aliwataka kupuuza propaganda zinazosambazwa na Maalim Seif na wenzake zenye lengo la kueneza chuki dhidi yake na viongozi wapya wa chama hicho ili wachukiwe na wasikubalike katika jamii na kuwataka kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali uchaguzi mkuu mwakani.

Awali, Makamu Mwenyekiti CUF Zanzibar, Abas Juma Muhunzi alisema Maalim Seif kwa miaka mingi alikigharimu chama hicho ikiwamo kuwapa watu nafasi kubwa wasiokua na uwezo kiutendaji.

Alisema mazingira hayo yamepelekea chama hicho kuwa na hali isiyoridhisha chini ya uongozi wake tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiri na kwamba sasa wanajipanga upya kukiimarisha chama hicho Zanzibar na Tanzania nzima.

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman alisema tofauti za vyama vya siasa isiwe sababu wa watu kutofautiana na kugombana badala yake kila mmoja afanye siasa bila ya kumbugudhi mwengine.

Advertisement