Lipumba amechagua kuizika CUF-chama ili aongoze CUF-jina

Muktasari:

  • Namkumbuka Lipumba wa mwaka 2001. Lipumba mwenye ari ya kupambana, mwenye kuikabili misukosuko ya kisiasa bila hofu wala kurudi nyuma. Lipumba mwenye moyo mkubwa kwa CUF, wanachama wake na nchi yake Tanzania.

Mambo ya CUF ni kizunguzungu tu. Profesa Ibrahim Lipumba amechaguliwa mwenyekiti na timu yake inapanga safu mpya ya uongozi, wakati huohuo, Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad na watu wake wanasubiri hatma ya kesi mahakamani.

Nianze kusema hivi namkubali sana Lipumba. Amekuwa mwanasiasa mzuri na mwenye kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa demokrasia nchini. Nyakati zote tangu mwaka 1995 alipochomoza kisiasa, amekuwa alama iliyokolea wino katika siasa za vyama vingi.

Alipogombea urais Tanzania kupitia CUF, mwaka 1995, akiwa kijana msomi mbobezi wa uchumi, aliikuta CUF na akakaribishwa. Wana-CUF wakampenda, wakamuamini. Wakamchagua kuwa mwenyekiti.

Kuanzia hapo akawa lulu ya kisiasa na kivutio cha wengi. Kuna wanasiasa wengi leo katika siasa za mageuzi, ama walivutiwa naye au walijengeka kutokana na harakati zake.

Namkumbuka Lipumba wa mwaka 2001. Lipumba mwenye ari ya kupambana, mwenye kuikabili misukosuko ya kisiasa bila hofu wala kurudi nyuma. Lipumba mwenye moyo mkubwa kwa CUF, wanachama wake na nchi yake Tanzania.

Baada ya maandamano ya Januari 26 na 27, 2001, Zanzibar na Dar es Salaam, CUF wakitaka watangazwe washindi wa Uchaguzi Mkuu 2000 na Seif atamkwe ndiye Rais wa Zanzibar, machafuko ya kihistoria yalitokea.

Wazanzibari wengi walipoteza maisha, maelfu walijeruhiwa na hata kupata ulemavu. Aibu kubwa zaidi ikawa kwa Tanzania kutengeneza wakimbizi waliokimbilia Mombasa na Lamu, Kenya. Kuna ambao walifika mpaka Somalia.

Lipumba akiwa anaongoza maandamano kwa Dar es Salaam; alikamatwa, alipigwa, alijeruhiwa na hata kutegeka mkono. Na akiwa na majeraha yake, aliwekwa mahabusu pamoja na wanachama, vilevile wafuasi wengine wa CUF.

Hii ni kuonesha kuwa yeye ni mwenyeji wa dhoruba za siasa za mageuzi kuliko wengi wanaoamini wameingia gharama kubwa kudai demokrasia. Gharama ambayo Lipumba ameilipia kwenye siasa za vyama vingi nchini haina fidia.

Kwanza naomba nieleweke kuwa mimi si mmoja wa wanaoamini kuwa Lipumba amehongwa fedha na CCM ili aivuruge CUF. Sina hulka ya kuamini na kushabikia mambo nisiyo na uhakika nayo.

Mimi nakubali kuwa Lipumba alikuwa sahihi kujiuzulu uenyekiti wa CUF mwaka 2015 kutokana na sababu zake mwenyewe. Vilevile naamini kuwa hakujirudisha mwenyewe CUF, bali aliombwa na wanachama.

Ni wazi kuwa baada ya Lipumba kujiuzulu na kuondoka, CUF haikuwa moja tena. Yaliibuka makundi mawili. Ndani ya chama hicho kukawa na timu za Zanzibar na Tanzania Bara.

Upande wa Bara ukajiona hauna nguvu, kwa hiyo ukaamua kumuita Lipumba ili arejee katika kiti chake. Naye akatumia mwanya wa kikatiba kwamba alijiuzulu lakini Baraza Kuu la chama ambalo ndiyo chombo kilichomchagua, halikukaa kuthibitisha kujiuzulu kwake.

Katika hali ambayo CUF inaelekea kaburini, Lipumba kama kweli anakipenda chama chake, angeweza kuchagua kukosa ili kibaki hai, na si kulazimisha anayolazimisha sasa, huku ikifahamika kwamba matokeo ni kukiua.

Lipumba anafahamu kuwa Wazanzibari kwa kadirio la asilimia 50, matumaini yao makubwa yanabebwa na CUF. Hili hawezi kuacha kulifahamu kwamba CUF kwa sehemu kubwa nguvu yake ipo Zanzibar. Unapoitaja Zanzibar moja kwa moja inafahamika kuwa nguzo ni Seif.

Kumwondoa Seif kwenye uongozi, maana yake ni kuiua CUF Zanzibar. Itabidi chama kianze kujipanga upya. Uchaguzi Mkuu 2020 au katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, CUF bila Seif, kitapata matokeo mabaya mno.

Ni kweli Msajili wa Vyama vya Siasa baraka zake zipo kwa Lipumba. Mamlaka za nchi zinatambua Lipumba ni mwenyekiti. Hata hivyo, chama ni mali ya wanachama. Katika uchaguzi, kura hupigwa na watu, mamlaka za nchi haziingizi kura kwenye masanduku.

Hata kama mamlaka hizo zinakuwa zimejitolea kumbeba Lipumba, lakini ni ukifika uchaguzi haziwezi kumsaidia apate kura nyingi, apate wabunge wengi kisha chama kipate ruzuku. Hilo halitatokea. Lipumba anafahamu kila kitu na ameamua kuizika CUF-chama ili abaki anaongoza CUF-jina.