Lishe ina uhusiano mkubwa na akili ya mtoto darasani

Sunday May 26 2019

Mratibu wa Mradi wa ASPIRES, Profesa David

Mratibu wa Mradi wa ASPIRES, Profesa David akizungumza kwenye Jukwaa la Fikra la Mwananchi lililokuwa likijadili Kilimo na Maisha Yetu, jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Said Khamis 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Licha ya Tanzania kujitosheleza kwa chakula, inaelezwa kuwa asilimia 34 ya watoto wanakabiliwa na udumavu ambao huchangia kudumaa kwa akili.

Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, udumavu ni ugonjwa wa utapiamlo unaosababishwa na mtoto kukosa lishe bora huku athari kubwa ikiwa kudumaa kwa akili katika masomo. Hivyo, lishe bora ina uhusiano mkubwa na uwezo wa mtoto darasani.

“Wakati mwingine unaweza kukimbizana na mtoto darasani kwa kuona hawaelewi kumbe ana tatizo la udumavu,” alisema mratibu wa mradi wa taasisi ya Aspires, Profesa David Nyange.

Profesa Nyange alikuwa akizungumza katika Jukwaa la Fikra la Mwananchi lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kwa ushirikiano na ITV na Redio One ambalo safari hii lilijadili kilimo, mratibu wa mradi wa taasisi ya Aspires, Profesa David Nyange alisema japo Tanzania inazalisha chakula kwa wingi lakini bado kuna tatizo la udumavu.

Utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) 2015/2016, unaonyesha kuwa kiwango cha udumavu nchini ni asilimia 34 huku mikoa inayozalisha chakula kwa wingi ikiongoza.

Utafiti huo unaonyesha kuwa mkoa wa Rukwa unaongoza kwa kuwa na asilimia 56.3 ukifuatiwa na mikoa ya Njombe na Iringa.

Advertisement

Profesa Nyange alisema kwa miaka 13, Tanzania imekuwa ikijitosheleza kwa chakula kutokana na juhudi kubwa zinazofanyika lakini pamoja na kuzalisha mazao kwa wingi, bado watoto wengi hawapati lishe bora.

“Kama mtoto hatapata lishe hataweza kukua kimwili na kiakili,” alisema Profesa Nyange.

Mtaalamu wa lishe wa Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Deborah Essau alisema akili ya binadamu huwa inatengenezwa katika siku 1,000 za kwanza tangu kuzaliwa.

“Msingi mkubwa ni siku 1,000 za kwanza na chini ya miaka mitano. Kama mzazi atakosea kwenye eneo hilo ni wazi kuwa atakuwa anamuandaa mtoto asiyeweza kufikiri kwa kina kwa sababu akili pia, hudumaa,” alisema Deborah.

Alisema kudumaa kwa akili ndio athari kubwa zaidi ya udumavu jambo linaloweza kumfanya mtoto ashindwe kumudu vyema masomo.

“Akili ya mtoto inapodumaa tarajia kupata matokeo hafifu darasani na ikiwa tatizo hili litaendelea kuwakumba watoto linatishia kutowapo kwa wataalamu wengi, siku zijazo,” alisema Deborah.

Kwa mujibu wa kitabu cha Baraza la Afya Duniani cha malengo ya lishe 2015, mtoto akidumaa hupata athari zisizoweza kurekebishika kwa sababu hudumu katika maisha yake yote.

Deborah alitaja athari nyingine kuwa ni kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi hali inayosababisha kupungua kwa tija na mapato ya kiuchumi.

Sababu za udumavu

Alisema kukosekana kwa lishe bora na kuugua mara kwa mara ndani ya siku 1,000 za kwanza husababisha kupata udumavu.

“Mtoto akizaliwa anashauriwa kupewa maziwa ya mama ndani ya miezi sita bila kupewa kitu kingine chochote lakini wengi hawafanyi hivyo,” alisema Deborah.

Alisema mtoto anapopewa chakula kidogo na kisicho na ubora, yaani virutubisho vinavyotakiwa, anakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata udumavu.

Deborah alisema lishe duni kwa wanawake kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua inachangia kwa kiasi kikubwa mtoto kupata udumavu ikiwa hatapata lishe bora.

Dalili za udumavu

Dalili kuu ya udumavu ni kuwa na kimo kifupi ukilinganisha na umri wake japo sio kila mtu mfupi ana udumavu.

Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Afya Duniani, Malengo ya lishe 2025, katika kila kundi la watoto watano wenye umri chini ya miaka mitano hapa nchini, wawili wamedumaa.

Nini kifanyike

Mtaalamu mwingine wa lishe kutoka Furaha Pamoja Foundation, Matrida Erick alisema ili kuboresha kiwango cha lishe nchini, lazima jamii ifundishe maana halisi ya lishe.

Aliwashauri wazazi kwenye mikoa inayozalisha chakula kwa wingi kutowasahau watoto kwa kuwa bize kwenye kilimo peke yake.

“Kwa sababu mikoa hiyo inalima mazao ya nafaka kwa wingi, waelimishwe ili waanze kufuga mifugo ya nyumbani kama kuku na kulima mboga za majani ili kupata lishe bora,” alisema.

Deborah alisema wanawake wanatakiwa kuhakikisha wanapata lishe bora kabla na baada ya kujifungua ili watoto wanyonye kwa kipindi husika huku wakipata maziwa yenye virutubisho.

Kwa nini mikoa yenye chakula ina udumavu?

Deborah alisema kuna sababu kadhaa zinazofanya mikoa yenye chakula kwa wingi kuwa na udumavu.

Alisema mikoa hiyo huzalisha nafaka zaidi hivyo watoto hupewa chakula cha aina moja kisicho na mchanganyiko wa virutubisho.

“Kwa mfano, wanazalisha mahindi, ngano ulezi, ndizi au muhogo. Asubuhi anaweza kumpa mtoto chai na muhogo, mchana ugali na maharagwe na jioni wakala ndizi. Hii ni aina moja tu ya chakula,” alisema Deborah.

Alisema wengi huamini kuwa lishe bora ni gharama dhana ambayo alisema si ya kweli.

“Wakati mwingine nyumba zenye tatizo la utapiamlo zinafuga kuku na kuna mayai, mboga za majani na matunda yapo lakini kilimo kimewafanya wazazi kuwa bize na kazi. Wanawasahau watoto,” alisema.

Alisema pia mila na desturi zinachangia kuwapo kwa udumavu kwa sababu umiliki wa mazao baada ya kukomaa huwa ni wa baba.

“Mwanamke anasaidia kulima ila wakati wa mavuno wanaume huvuna na kuuza chakula chote, hapo mama anaanza tena kuhangaika,” alisema.

Ofisa mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Usia Nkoma alisema inawezekana kumaliza tatizo la udumavu kwa watoto ikiwa jamii itawekeza kwenye lishe bora.

“Hata ule unga uliochanganywa nafaka zote unaoitwa wa lishe si lishe. Huwezi kuchanganya nafaka tofauti zinazoiva tofauti na kumwandalia mtoto ukisema ni lishe, si sahihi” alisema Usia.

Alisema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kumaliza tatizo hilo na sasa wapo kwenye mikoa ya Rukwa, Iringa, Njombe na Songwe.

Advertisement