Lissu: Nimelipwa mshahara, nitadai gharama za matibabu mahakamani

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema Bunge limemlipa mshahara na posho alizokuwa akidai, lakini bado hajalipwa stahiki za matibabu ambazo atakwenda kuzidai mahakamani.

Februari 12, Lissu alisema amesitishiwa mshahara na stahiki zake za kibunge na kwamba endapo Spika na Katibu wa Bunge hawatamlipa atakwenda kudai mahakamani.

Baada ya kauli hiyo ya Lissu, Spika Job Ndugai alisema mnadhimu mkuu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni asingeweza kulipwa fedha za walipa kodi wakati akiendelea kuisema vibaya nchi yake nye ya nchi. Kipindi hicho Lissu alikuwa ziarani Marekani.

Aprili 7, kiongozi huyo wa Bunge alilieleza Mwananchi kuwa Lissu ambaye yuko Ubelgiji akiendelea na matibabu amekwishalipwa madai yake yote.

Lissu amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na kati ya hizo 16 zilimpata mwilini katika makazi yake Area D jijini Dodoma.

Jana, Lissu alitoa ujumbe aliousambaza kwenye mitandao ya kijamii akieleza malipo yake yaliyositishwa na baadaye akatoa ufafanuzi alipozungumza na Mwananchi kuhusu madai ya gharama za matibabu.

“Kwa kifupi ni kwamba Spika Ndugai na watu wake wamelipa mshahara wangu wa tangu Januari hadi Machi waliokuwa wameuzuia.

“Kwa maoni yangu, kilichowafanya wakubali yaishe ni ujasiri wa watu wengine mlioamua kunichangia, siyo tu gharama za matibabu yangu, bali hata huo mshahara uliozuiliwa kinyume na sheria na kanuni za Bunge,” alisema Lissu katika ujumbe aliousambaza mitandaoni.

“Sikukubali kufa kimyakimya na ninyi ndugu zangu hamkukubali. Walipoona sokomoko la mshahara wangu limekuwa kubwa na sasa limebebwa na wananchi, wakakubali yaishe. Nawapongezeni sana kwa ushindi huu.

“Hili ni funzo kubwa sana kwa kila mmoja wetu. Tusikubali kukaa kimya tunapoonewa. Hakuna fedheha yoyote katika kupiga kelele za kudai haki. Tupaze sauti zetu na kupiga kelele, watu wema watasikia kilio chetu na tutapata msaada.”

Akijibu swali kama bado anakusudia kwenda mahakamani alisema “nilisema nitaenda mahakamani kama hawatalipa mishahara na posho zangu za kibunge, kama wameshanilipa suala la kwenda mahakamani halipo tena.”

Mwananchi lilipotaka kujua kama gharama za matibabu nazo zimelipwa kama ambavyo amekuwa akitaka alipiwe na Bunge, Lissu alisema hazijalipwa na bado anazidai.

Aliwataka Spika Ndugai na Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai wajiandae akisema, “mie ndiye mlalamikaji na shahidi muhimu, ni muhimu niwepo mahakamani. Kwa hiyo kesi hiyo inasubiri kurudi kwangu.”

Kuhusu maendeleo ya afya yake, mwanasiasa huyo alisema anaendelea vizuri. “Napenda wananchi wangu wa Singida Mashariki wafahamu kwamba mwaka huu hautafika mwisho kabla sijarudi nyumbani, Inshaallah.”

Alisema Aprili 2 alikutana na madaktari wake kwa mara ya kwanza tangu alipofanyiwa operesheni Februari 20 na anachokifanya kwa sasa ni mazoezi ya kutembea. “Taarifa yao ni kwamba mfupa wote wa mguu wa kulia umepona vizuri. Sehemu iliyowekewa ‘kiraka’ cha mfupa na kupigwa ‘ribiti’ ya chuma juu kidogo ya goti, na sehemu ya kwenye paja iliyotakiwa kuota mfupa mpya, zote ziko vizuri,” alisema.

Pia, mnadhimu huyo wa upinzani bungeni alisema Mei 14 atapimwa urefu wa miguu ili atengenezewe kiatu au soli maalumu kwa ajili ya mguu wa kulia.

“Kwa sababu ya majeraha makubwa niliyopata, mguu huo ni mfupi kwa sentimita kadhaa. Bila kiatu au soli maalumu nitakuwa ‘langara’ sana na madaktari wamesema hiyo si sawasawa.”

Alisema, “sasa nina tarehe ambayo madaktari wangu wamesema nitakuwa ‘fiti’ kurudi nyumbani. Msiniambie niiseme kwa wakati huu. Tunahitaji kushauriana na wadau mbalimbali kuhusu tarehe halisi na namna bora zaidi ya kurudi kwangu nyumbani.”

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Spika Ndugai alisema mhimili huo umeshamlipa Lissu madai yake yote huku akimtaka kama ana jambo lolote kuwasiliana na mamlaka husika, si kutumia mitandao ya kijamii.

Ndugai alitoa kauli hiyo siku 10 tangu Lissu kumwandikia barua katibu wa Bunge, Kagaigai, akimtaka kumlipa mshahara na posho zake za kuanzia Januari, ndani ya siku 14 vinginevyo atakimbilia mahakamani.

Machi 27, Kagaigai alipoulizwa kama amepata barua hiyo alisema hajaipata lakini wakili wa Lissu, John Mallya alisema alituma barua hiyo kwa njia mbili. Moja ilitumwa ofisi ndogo ya Bunge Dar es Salaam kwa njia ya kitabu cha hati ya kupokea kwa kutia saini (dispatch) na nyingine kwa EMS.

Katika maelezo yake, Ndugai alisema Lissu anatumia njia zisizo nzuri sana kueleza masuala yake, likiwamo hilo la madai yake.

“Hii si njia nzuri ya mawasiliano, ninachosisitiza mtu ni mtumishi katika taasisi unatakiwa kuwajibika kwa watu fulani fulani lakini huwatambui huwasiliani nao,” alisema Ndugai.

Alisisitiza, “Nimesema hana anachodai, akiona (Lissu) imepita wiki moja kuna anachodai arudi tena (kufuatilia).”

Awali, Ndugai alisema kama kweli Lissu ana haki zake zitalipwa na huenda zimeshalipwa huku akisisitiza kuwa jambo hilo ni dogo.

Alimshauri Lissu kutafuta ufumbuzi wa masuala yake ya bungeni kupitia viongozi mbalimbali wa upinzani.