Lissu ataja sababu za kurejea nchini Septemba 7 Mbowe akoleza ujio wake

Muktasari:

Tundu Lissu ametosa sababu mbili za kuitumia siku ya Jumamosi ya Septemba 7 mwaka huu kurejea nchini baada ya kuwa nje kwa miaka miwili huku mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema maandalizi ya ujio huo yameanza.

Dar es Salaam. Tundu Lissu ametosa sababu mbili za kuitumia siku ya Jumamosi ya Septemba 7 mwaka huu kurejea nchini baada ya kuwa nje kwa miaka miwili huku mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema maandalizi ya ujio huo yameanza.

Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa eneo la makazi yake Area D, Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali akiwa hajitambui kisha usiku wa siku hiyo alisafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Lissu alitibiwa Nairobi mpaka Januari 6 mwaka jana kisha alihamishiwa nchini Ubelgiji ambako yupo mpaka sasa akipatiwa matibabu.

Mwanasiasa huyo aliyefanyiwa upasuaji zaidi ya mara 20 katika hospitali zote tatu za Dodoma, Nairobi na Ubelgiji ametoa sababu ya kurejea nchini Septemba 7. “Madaktari wangu wamenipa ahadi ya kukutana nao Agosti 20 na baada ya hapo nitapata ruhusa, sasa baada ya hapo nitakuwa nasubiri kuonana nao kila mwaka.”

Pili, alisema “Septemba 7 niliondoka Tanzania nikiwa nusu mfu, kuna watu walitaka nife hivyo nimeamua Septemba 7 iwe safari yangu ya kurudi Tanzania nikiwa mzima ili kudhihirisha hao waliotaka kuniua kuwa niko hai.”

Sababu hizo mbili zinaungwa mkono na Mbowe aliyesema Septemba 7 ni siku muhimu na maalumu kwa wapigania demokrasia na haki za binadamu.

“Septemba 7 ni siku maalumu sana, ilikuwa pigo kwa demokrasia, uhuru wa wapigania haki za binadamu kwa kushuhudia tukio la mwenzao anashambuliwa hadharani tena mchana kweupe, ndio sababu Lissu anarejea Septemba 7,” alisema Mbowe.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema “maandalizi yanafanyika ya ujio wake, muda ukifika Watanzania wataelezwa itakuwaje lakini kwa sasa itoshe kujua tu kuwa Lissu atarudi Septemba 7.”

Alute Mughwai ambaye ni kaka yake Tundu Lissu alisema, “kama ambavyo Lissu mwenyewe alisema akipona na madaktari wakimruhusu atarejea, tunamsubiri kwa hamu kwani kama tulivyommisi sisi na Watanzania wote. Tunamkaribisha sana.”

“Nitarudije, itakuwaje, safari itakuwaje hizo ni taratibu ambazo hatuwezi kuziweka wazi kwa sababu muda ukifika Watanzania watajulishwa,” alisema Lissu.

Baadhi ya wabunge, Goodluck Mlinga (Ulanga-CCM), John Heche (Tarime Vijijini-Chadema) na Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ (Mtera-CCM) walisema wanamsubiri mbunge mwenzao.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Lissu akijibu swali kuwa atarejea na dereva wake alisema, “hilo ni jukumu lake, yeye ni mtu mzima, ataamua yeye. Lakini anahitajika naye kuhakikishiwa ulinzi wake.”

Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba, 2019 atashiriki.