Lissu kufanyiwa kipimo cha mguu ili kutengenezewa kiatu

Thursday April 25 2019

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu 

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mdhamini wa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mbunge huyo anaendelea  vizuri lakini bado yupo hospitalini akiendelea na matibabu nchini Ubeljiji.

Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano katika Mahakama hiyo, likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume cha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Hata hivyo, Lissu yupo nje ya nchi kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017 jijini Dodoma.

Mdhamini huyo, Robert Katula ameieleza Mahakama hayo leo Aprili 25 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Katula alieleza amepewa taarifa kutoka kwa daktari anayemhudumia  Lissu kuwa Mei 14  madaktari watamfanyia  vipimo vya mgumu ili aweze kutengenezewa kiatu kutokana na mguu moja uliopata  majeraha ya risasi kuwa mfupi.

"Lissu  bado anaendelea na matibabu huko nchini Ubeljiji lakini anaendelea vizuri na nilipewa taarifa kuwa Mei 14 mwaka huu madaktari  watamfanyia vipimo vya mguu  kwa ajili ya kumtengenezea kiatu" alisema Katula.

Awali, wakili wa Serikali Dhamiri Kasinde alidai kuwa kesi hiyo ilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa, hivyo kutokana na mshtakiwa kuwa mgonjwa aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 23 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 208/2016 ni mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Washtakiwa hao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume ncha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa, Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hiyo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo manispaa ya Ilala alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa msajili wa magazeti.

Advertisement