Lissu kurejea Tanzania Septemba 7, kushiriki uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema atarejea Tanzania Septemba 7, 2019 siku ambayo atatimiza miaka miwili tangu aliposhambuliwa kwa risasi jijini Dodoma  Septemba 7, 2017.

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema atarejea  Tanzania Septemba 7,  2019 kutoka nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu.

Lissu amekuwa nje ya Tanzania tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana  akiwa eneo la makazi yake Area D, Dodoma.

Mara baada ya kushambulia, mwanasiasa huyo  alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopata matibabu hadi Januari 6, 2018 na kuhamishiwa  Ubelgiji kuendelea na matibabu zaidi.

Lissu ambaye kwa sasa anatembea kwa msaada wa gongo moja akizungumza na wapiga kura wake mwishoni mwa wiki kupitia simu ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema anarudi nchini Septemba 7, 2019.

Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyila (TLS) amesema katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba, 2019 atakuwepo Tanzania.

Akizungumza na Mwananchi  leo Jumatano Mei 22, 2019 Mnadhimu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema, "Narudi nyumbani Septemba 7 ya anniversary ya kushambuliwa kwangu."