Lori lakamatwa na maguni 200 ya mahindi

Wednesday March 6 2019

 

By Nazael Mkiramweni na Rachel Chibwete [email protected]

Dodoma. Lori la wizi lenye namba za usajili T 519 CPB na tela namba T 544 CBF limekamatwa jijini Dodoma likiwa na magunia 200 ya mahindi huku likidaiwa kufanya matukio ya wizi zaidi ya manane katika maeneo mbalimbali nchini.

Lori hilo aina ya Iveco liliibwa Oktoba 26, 2018 likiwa na mzigo wake uliokuwa ukisafirishwa kwenda DRC – Congo likiwa na namba za usajili T 506 BXD na tela lake T 619 CVZ.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto jana Machi 5, 2019 jijini hapa alisema baada ya gari hilo kuibwa kesi ilifunguliwa Kijitonyama Dar es salaam na katika ufuatiliaji wa awali ilibainika gari lenye namba ambazo lori hilo lilikutwa nazo lipo jijini Dar es Salaam likiwa ni mali ya kampuni ya Shaimark.

Muroto alisema ufuatiliaji huo ulibaini gari hilo limekuwa likibadilishwa namba mara kwa mara, hivyo kufanikiwa kuiba mali za watu katika maeneo tofauti.

“Waliiba mbolea, waliiba tambi, waliiba ngano iliyokuwa ikisafirishwa kwenda Tunduma, waliiba chumvi iliyokuwa ikisafirishwa kwenda Lindi na Mpanda, waliiba shehena ya mahindi Singida, waliiba shehena ya mbaazi Kongwa - Dodoma, waliiba mbao Mbeya lakini pia waliiba mahindi ya serikali Makambako mkoani Njombe,” alisema Muroto.

Kamanda Muroto aliwataja watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo kuwa ni Emmanuel Kitinye (42), mkazi wa Ubungo Kibangu Dar es Salaam ambaye alikamatwa na leseni mbili ambapo nyingine ina jina la Michael Ngoh pamoja na Idrissa Nassoro (35) mkazi wa Ubungo.

Advertisement

Katika tukio lingine kamanda huyo alisema wamekamata bastola iliyokuwa imezikwa katika eneo la Iringa Road iliyotelekezwa kutokana na wananchi kuogopa kukamatwa katika operesheni wanazoendelea kuzifanya, hivyo wahusika waliamua kuitelekeza eneo hilo.

Muroto aliwataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume na sheria kuziwasilisha polisi kabla hawajakamatwa.

Advertisement