Lowassa, Gambo washiriki mazishi ya kiongozi mkuu wa mila Wamasai

Monduli. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, jana waliungana na viongozi wengine pamoja na wananchi katika mazishi ya kiongozi mkuu wa mila wa jamii ya Wamasai, Mepukori Mberekeni.

Mazishi hayo yaliyofanyika katika Kijiji cha Mti Mmoja wilayani hapa, pia yalihudhuriwa na Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga na Mkuu wa wilaya hiyo, Rashid Taka.

Kiongozi huyo alifariki dunia Januari Mosi, mwaka huu katika Zahanati ya Mti Mmoja.

Katika salamu zake, Lowassa alisema wakati wa uhai wake Mberekeni alikuwa kiongozi aliyejihusisha kuhamasisha amani na utatuzi wa migogoro ya ardhi katika jamii ya wafugaji.

“Alitumia kipawa chake vizuri na alikuwa kiongozi mahiri katika jamii yetu kwa kuiunganisha na kuhakikisha tunaishi kwa upendo,” alisema Lowassa.

Mrisho Gambo ambaye yupo kwenye ziara ya kuhamasisha ujenzi wa madarasa wilayani humo, alisema Mberekeni atakumbukwa kwa kupenda elimu wilayani humo.

“Niwape pole familia hii kwa msiba uliowakuta, Serikali siku zote imekuwa ikishirikiana na viongozi wa mila kuhamasisha maendeleo na amani,” alisema Gambo.

Laigwanani mkuu wa Wamasai nchini, Lekisongo Meshuko Meijo alisema jamii hiyo imepata pigo kubwa.

Aliitaka jamii na familia ya marehemu kudumisha amani na utulivu kwa kuendeleza mema yote aliyoyaacha. Mberekeni alizaliwa Aprili 15, 1959, ameacha wajane wawili, watoto 17 na wajukuu tisa.