UCHOKOZI WA EDO: Lowassa ametuziba wote midomo, tunaona aibu

Maisha bila ya unafiki hayaendi. Niliwahi kusema zamani. Jaribu kumtazama baba yangu, Edward Lowassa. Amenifkirisha. Amenifikirisha kweli kweli. Hajawahi kuwa mbaya wala mzuri kwa pande zote mbili alizowahi kuchezea. Simba na Yanga.

Kule alikohama hivi karibuni zamani walikuwa wanamshutumu. Walidai hafai kabisa. Waliwahi kumuweka katika orodha ya watu wasiofaa nchini. Baadaye upepo ukabadilika. Akafaa. Hawakusema tena kwamba hafai. Walikaa kimya. Hata kama hawakumtetea sana lakini hawakusema kama hafai.

Kazi ya kudai hafai ikahamia kwa wale ambao awali walisema anafaa. Kicheksho kweli kweli. Wakaulizwa, kama alikuwa hafai kwa nini hamkusema mpaka alipokuja kwetu? Kwa nini hamkukubali madai yetu wakati ule tuliposema hafai? Tuachieni. Sisi anatufaa.

Baadaye upepo umebadilika tena. Amerudi kule kwa zamani kwa wale ambao miaka mitatu iliyopita walisema hafai ingawa zamani walisema anafaa. Majuzi nikamuona wajina wangu akipokewa kwa vigeregere pale Lumumba. Baadaye akapokewa kwa misafara Monduli. Kichwa kikaanza kuniuma.

Sasa picha imerudi kama zamani. Wale waliwahi kusema anafaa, kisha hafai, sasa inabidi waanze kazi ya kusema anafaa. Wale ambao waliwahi kusema hafai, kisha anafaa, sasa inabidi waanze kazi ya kusema hafai.

Hata hivyo, ninachoona kwa sasa kazi hizi za sasa zinafanywa kwa aibu kidogo. Upande wa kule unaogopa kummwagia sifa sana wakihofia kukumbushwa maneno yao ya kashfa wakati wa uchaguzi, na upande huu mwingine unaona aibu kumponda sana wakihofia kukumbushwa sifa walizommwagia wakati wa uchaguzi. Ngoma droo.

Ninachoona ni kwamba ametufunga midomo. Sijui hali itakuaje mbele ya safari. Sijui atatumikaje wakati wa uchaguzi lakini hata sisi tulioishia darasa la saba tutajitokeza kuziambia pande zote zifunge midomo. Hakuna upande ambao haujawahi kumwita wajina wangu shujaa na hakuna upande ambao haujawahi kumwita fisadi.

Wanadamu wa pande zote mbili hizi wamebakia kuwa wanafiki tu. Washindi ni sisi watu tusiokwenda shule ambao tumeamua kufanya vibarua vyetu na kutafuta mlo wa familia ili kujenga nchi. Siasa hazitaijenga nchi hii hata siku moja.

Siku tukiwa makini na mambo ya msingi tukapuuza siasa nadhani tutafika mbali. Kitu ambacho watu walio katika siasa wanaweza kusema kweli ni salamu tu.