VIDEO: Ludovick Utouh afunguka mvutano wa CAG, Bunge

Muktasari:

Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema CAG ni jicho la wananchi ambao ndiyo wenye mali na rasilimali zote za nchi hivyo ripoti inakwenda bungeni sababu waliopo ndani yake ni wawakilishi wa wananchi na kwamba mapendekezo yake hulenga kuboresha utendaji wa aliyemkagua.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema mabishano yaliyotokea bungeni kati ya Bunge dhidi ya CAG, Profesa Mussa Assad ni kukosekana kwa wabunge wenye utaalamu wa kutosha wa taaluma ya uhasibu ndani ya Bunge, hali iliyochangia lugha kutoeleweka.

Amesema CAG ni jicho la wananchi ambao ndiyo wenye mali na rasilimali zote za nchi na kwamba ripoti inakwenda bungeni sababu waliopo ndani yake ni wawakilishi wa wananchi na kwamba mapendekezo yake hulenga kuboresha utendaji wa aliyemkagua.

Utouh ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku mbili la Chama cha Wahasibu wanawake Tanzania (TAWCA).

“Wangekuwapo wataalamu wa kutosha wa fani ya uhasibu bungeni, wangeongea lugha moja na CAG kwa kutambua kile alichokizungumza na maana yake, mwaka huu na mwakani ni kipindi cha uchaguzi jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi hizo msisubiri uteuzi,” amesema akiwahamasisha washiriki wa kongamano hilo na kuongeza:

“Isitoshe mwanamke kuwa mtaalamu tu, fikirieni kuingia katika nafasi za siasa kwa sababu siasa ndiyo zinatengeneza sheria, kanuni za uendeshaji wa nchi kuna nafasi kwa kinamama kuchangia katika hilo.”

“Naiomba Serikali na sekta binafsi waangalie umuhimu wa kuwaweka kina mama katika nafasi za uongozi, tafiti katika nchi nyingi duniani zimeonyesha kuwa kinamama wahasibu wanafanya vizuri kuliko kinababa.”

Awali, Mwenyekiti wa TAWCA, Neema Kiure-Mssusa amesema mkutano huo unawakutanisha wanawake wahasibu 300 kwa lengo la kujadili changamoto na mwelekeo katika fani hiyo.

“Tutaangalia jinsi ya kutatua changamoto na kubwa wengi hawaombi kutumikia nafasi zingine lakini ukweli ni kwamba tuna nafasi kubwa ya kuleta chachu katika nchi hasa katika Tanzania ya viwanda,” amesema.